Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amemkabidhi hati ya jengo la bunge kwa Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai mapema leo.
Aidha Lukuvi amemshukuru Mhe. Spika kwa kutilia mkazo maagizo ya Serikali kwa taasisi zake ya kupima na kuchukua hati zao ili kuyalinda maeneo yao na kuepusha migogoro na wananchi.
Mhe. Lukuvi pia ametumia nafasi hiyo kuzitaka taasisi nyingine za Serikali kuhakikisha zinapima na kuchukua hati za maeneo wanayoyamiliki. Upimaji huo unaweza kufanywa na wapima wa serikali au wapima binafsi ambao wamesajiliwa na Wizara ya Ardhi.
Akiipokea hati hiyo huku tukio hilo likishuhudiwa na Katibu wa Bunge Ndg. Stephen Kagaigai, Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai (Mb) alisema kwamba sasa badala ya kuwa wapita njia na wapangaji kwa hati hizi anaamini wapo nyumbani.
“Nami nitoe wito kwa Taasisi zote za kiserikali Wizara na Mashirika kuhakikisha kwamba maeneo yao yote yamepimwa na yana hati” Alisema Spika Ndugai.
Kwa upande wa wananchi, Mhe. Waziri Lukuvi amewataka wale ambao maeneo yao hayajarasimishwa wafanye hivyo kulinda milki zao na wale wanaomiliki kisheria wahakikishe wanalipa kodi zao kwa wakati kuepusha usumbufu utakaotokana na limbikizo la kodi hizo.
Wizara ya ardhi itaendelea kutoa ushirikiano kupitia Ofisi zake zilizoanzishwa kila mkoa ili kurahisisha upimaji na upatikanaji wa hati kwa taasisi za serikali na jamii yote kwa ujumla.