NEWS

7 Mei 2021

161 Wakamatwa Kwa kujihusisha na wizi wa pikipiki na magari

 


Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata watu 161 wanaotuhumiwa kujihusisha na wizi wa pikipiki, magari na vifaa vyake.

Kukamatwa kwa watuhumiwa hao ni matokeo ya operesheni iliyofanywa na polisi kuanzia Aprili 20, 2021 baada ya kuwepo kwa malalamiko ya wamiliki wa vyombo hivyo vya moto kutoka maeneo mbalimbali.

Kutokana na taarifa iliyotolewa Mei 6, 2021 na kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema wamefanikiwa kuwakamata vinara watano wa wizi huo.

“Katika idadi ya watuhumiwa hao 161, kuna watuhumiwa watano vinara wa wizi wa pikipiki, wamekamatiwa Zanzibar wakiwa na pikipiki 40 za wizi. Watuhumiwa hawa wamekuwa wakiiba pikipiki hapa jijini Dar es Salaam, Morogoro na Pwani na kuzipeleka Zanzibar kutafuta wateja,” amesema Mambosasa.

Mambosasa amesema katika taarifa hiyo kwamba watuhumiwa hao vinara wataletwa Dar es Salaam kutoka Zanzibar pamoja na vielelezo na watafikishwa mahakamani baada ya kukamilisha taratibu zote za kisheria.

Katika operesheni hiyo, polisi wamefanikiwa kukamata magari mawili, moja ni aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T 770 ACY na Toyota IST lenye namba T 137 DMM. Magari hayo yote yaliibiwa Aprili na kupatikana Mei, 2021.