Rais wa Kenya, Uhuru Kenyata ametoa wiki mbili kwa watendaji serikalini kuhakikisha sakata la mahindi ya Tanzania yaliyozuiwa kuingia Kenya linapatiwa ufumbuzi.
Kenyata ametoa agizo hilo leo Jumatano Mei 5, 2021 mjini Kenya katika kongamano la wafanyabiashara mbele ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
Katika maelezo yake Kenyatta amesema Kenya na Tanzania ni nchi jirani na ndugu, hakuna sababu ya kuwekeana vikwazo vitakavyoumiza wananchi.
“Natoa maelekezo hapa, kwanza yale mahindi yaliyolala mpakani waziri nakupa wiki mbili hilo suala liwe limeisha. Pili mawaziri wanaohusika nendeni kutatua foleni iliyopo Taveta na Holili, kama suala ni vyeti vya Covid 19 hakuna haja ya mtu wa mataifa haya kupimwa mara mbili kama amechekiwa Tanzania basi aingie Kenya,” amesema Rais Kenyata
Pia amewataka wawekezaji kutoka Tanzania kuwa huru kufanya biashara zao Kenya akiahidi Serikali yake kuendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na ufanyaji biashara.