Samirah Yusuph
Bariadi, Ungwe ya pili ya mgogoro kati ya wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu, wenye mashamba na wamiliki wa leseni katika mgodi mdogo wa Bulumbaka wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu umeshika hatamu baada ya ule wa kwanza kumalizika.
Mgogoro huu unajumuisha leseni tatu zinazopingwa na wamiliki wa mashamba pamoja na wachimbaji wadogo huku leseni moja tayari kesi yake ipo katika mahakama ya wilaya ya Bariadi.
Tangu kuanza kwa mgogoro huo takribani majuma mawili wachimbaji wamesitisha shughuli zote za uchimbaji na uuzaji wa mawe jambo ambalo wamelitaja kuwa linaathiri uchumi wao na wa vibarua wao kwa sababu mzunguko wa pesa umesimama.
"Waruhusu mgao ili tupate pesa tunapata hasara kwa sababu tayari tumewekeza na hakuna kinacho ingia katika uwekezaji huo...
Chanzo cha mgogoro ni ofisi ya madini kugeuka kuwa madarali katika utoaji wa leseni kwa sababu serikali ilielekeza utaratibu wa kupata leseni unajumuisha wamiliki wenye mashamba pamoja na wawekezaji watakaohitaji leseni," alieleza Denis Clement mchimbaji mdogo katika mgodi wa Bulumbaka.
Wachimbaji hao pia wamelalamikia pia zoezi la uwekaji alama katika viroba ili kuvitoa mgodini kuwa limegubikwa na mashaka kwasababu hakuna bei elekezi hivyo kutozwa pesa kulingana na uhitaji wa mtozaji pamoja na kulipa walinzi japo suala la ulinzi lipo chini ya mmiliki wa leseni.
Katika ufumbuzi wa mgogoro huo mkuu wa wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga amefika mgodini hapo na kusitisha leseni tatu ambazo zinamgogoro pamoja na kuwataka wamiliki wa leseni hiyo kufika katika ofisi ya mkuu wa wilaya ili kuhakiki uharali wa leseni hizo.
"Ni marufuku kufanya kazi kwa leseni ambazo zinakuja mgongo wa nyuma katika migodi ya Bariadi...Leseni zote zifuate utaratibu wa kisheria ili haki ipatikane kwa kila mmoja, uwajibikaji na uwazi vitamaliza mgogoro huu ambao hakuna sababu ya kuendelea kuulea," alisema Kiswaga.
Mgodi wa Bulumbaka ni miongoni mwa migodi mitatu iliyopo katika wilaya ya Bariadi ambayo ni Dutwa one na Dutwa two.
Mgogoro huu unaibua taswira mpya ya ukiukaji wa maelekezo yaliyotolewa na waziri wa madini Dotto Biteko Desemba 19,2020 alipokuwa katika ziara ya siku moja mkoani Simiyu baada ya kuibuka kwa malalamiko ya wachimbaji wadogo dhidi ya wamiliki wa leseni katika migodi iliyopo mkoani humo.
Katika ziara hiyo Biteko alitoa maelekezo ya utoaji wa leseni kuwa ni pamoja kuwashirikisha wamiliki wa mashamba katika mchakato wa kuomba leseni ili kuondoa migogoro itakayo sababishwa na ukiukaji wa kanuni za upatikanaji wa leseni.
Mwisho.