NEWS

5 Mei 2021

Majaliwa: Wana-Buhigwe Tumchague Kavejulu Ana Uwezo Wa Kututumikia

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa amewaomba wakazi wa jimbo la Buhigwe wamchague Eliadory Kavejulu kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa kuwa ndiye mwenye uwezo na nia ya dhati ya kuwatumikia.

 “Wana-Buhigwe wote bila ya kujali vyama vyenu nawaomba kura zenu. Tarehe 16 itakapofika mumpigie kura mgombea wa CCM, kwani mnapomchagua muwakilishi si wakati wa kuleta mzahazaha lazima tumchague mtu atakayekuwa tayari kututumikia”.

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumatano, Mei 5, 2021) alipozungumza na wakazi wa  jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge uliofanyika katika uwanja wa shule ya msingi Buhigwe.

Amesema CCM pekee ndicho chama cha siasa nchini chenye ilani na kinachoweza kuwatumikia na kuwahudumia Watanzania wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote, hivyo amewaomba wanaCCM na wa vyama vingine wamchague mgombea wa CCM ili aweze kuwaletea maendeleo.

Amesema mgombea wa CCM ambaye kitaaluma ni mwalimu, akichaguliwa atashirikiana na wakazi wa jimbo hilo katika kusimamia na kuboresha maendeleo ya sekta mbalimbali ikiwemo ya elimu. “Mwalimu Kavejulu ndiye mwenye uwezo wa kuwaletea maendeleo”.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, ameongeza kuwa wakazi wa jimbo hilo wamchague Kavejulu ili aweze kusimamia vizuri miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali katika jimbo hilo ikiwemo ya ujenzi wa barabara, maji na afya.

Naye, mgombea wa ubunge katika jimbo hilo, Mwalimu Kavejulu ametumia fursa hiyo kuwaomba wakazi wa jimbo hilo kumpigia kura nyingi za ndio ili aweze kuwa muwakilishi wao atakayeshirikiana nao katika kuhakikisha jimbo hilo linaendelea kupata maendeleo.

“Msiwe na shaka ya aina yoyote mahitaji yote ya kata zote 20 nayajua, naomba munichague nikayafanyie kazi. Nitawashirikisha wadau wa masuala mbalimbali wakiwemo wa kilimo ili tuweze kupanga namna ya kuboresha kilimo chetu. Ukinichagua umechagua maendeleo”.

Kwa upande wake, aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo Albert Obama amewaomba wakazi wa jimbo Buhigwe wamchague Mwalimu Kavejulu kwa sababu ni kiongozi mwenye uwezo mkubwa wa kuwatumikia. “Tumchague Kavejulu hata kwama popote”.