NEWS

8 Mei 2021

Mbaroni Kwa Kuua Mke Kisa Anatumia (ARV’s) Kwa Siri

 


SALVATORY NTANDU
Mkazi wa mtaa wa Dome kata ya Ndembezi halmashauri ya manispaa ya Shinyanga, Peter Elias (29) anashikiliwa na Jeshi la polis kwa tuhuma za kumuua  mke wake aliyefahamika kwa jina la Pili Luhende baada ya kubain anatumia dawa wa kufubaza makali ya virusi vya ukimwi (ARV’s) kwa siri.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa taarifa kwa vyombo vya habari na kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga (ACP) Debora Magiligimba imesema kuwa tukio hilo limetokea Mei 3,mwaka huu majira ya saa nne na nusu usiku nyumbani kwake ambapo Peter alitekeleza mauaji hayo.

Kamanda Magiligimba alisema kuwa walipokea taarifa za  Pili Luhende, kupigwa na kisha kuuawa na mume wake hadi kupoteza maisha ambapo makachero wa polisi  walifanikiwa kumkamata Peter na kumhoji ndipo ambapo alipokiri kutekeleza mauaji hayo .

 “Mnamo Mei 6 mwaka huu  Peter alikubali kuonesha mwili wa mke wake alipoutelekeza baada ya kufanya mauaji hayo katika eneo la mwagala darajani na alikiri kutekeleza mauaji hayo baada kubaini mwenza wake anatumia za (ARV’s) kwa siri ndipo alipopata hasira na kumpiga ngumi hadi kupoteza maisha,”alisema Magiligimba.

 Kamanda Magiligima alisema kuwa mwili wa marehemu umekutwa ukiwa umeharibika na umekabidhiwa kwa ndugu zake  ajili ya taratibu za mazishi  na  mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

“Nitoe  wito kwa wanandoa  mkoani Shinyanga kuacha tabia ya kuchukulia sheria mkononi kwa wenza wao na badala yake wapeleke malalamiko yao kwenye madawati ya jinsia na watoto yaliyopo vituo vya polisi au ustawi wa jamii ili kupata suluhisho la migogoro yao,”

Mwisho.