Na Benny Mwaipaja, Dodoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameishauri Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kusimamia kikamilifu sekta ya mifugo kwa kubuni njia mbalimbali zitakazoongeza tija katika sekta hiyo.
Dkt. Nchemba ametoa ushauri huo Jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Wizara hiyo pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii, kujadili masuala mbalimbali yanayohusu namna ya kuboresha sekta ya mifugo ili iweze kuongeza mchango katika ukuaji wa uchumi wa nchi na maendeleo ya watu.
“Tutakavyo weka mipango ya kisasa ya kukuza uzalishaji katika eneo hili la mifugo, tutatengeza wigo mkubwa wa walipakodi, tutabadilisha maisha ya watu wetu, tutakuza uchumi na ajira” alisema Dkt. Nchemba
Alisema kuwa maendeleo ya sekta ya viwanda yanayokwenda kwa kasi hapa nchini yanahitaji malighafi za kulisha viwanda hivyo na kwamba fursa zilizopo kwenye sekta ya mifugo ni kubwa na kushauri mbinu za kisasa za kuendeleza ufugaji ziwekwe bayana na kufanyiwa kazi ipasavyo.
Alisema utaratibu wa sasa wa wafugaji kuhamahama na mifugo kwa ajili ya kutafuta malisho na maji umepitwa na wakati na kuahidi kuwa Wizara yake iko tayari kutoa ushirikiano ili kufanikisha mipango ya kuendeleza sekta ya mifugo nchini.
Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki, alimshukuru Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango kwa kukutana na vingozi wa Wizara hizo mbili na kuahidi kuwa ushauri uliotolewa utafanyiwa kazi kikamilifu ambapo ameunda timu ya wataalamu kwa ajili ya kuchambua mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa katika kikao hicho alichosema kilikuwa ni cha muhimu.
“Tutaangalia namna ya kupanua na kuwa na maeneo maalum ya malisho ya mifugo yetu pamoja na kuboresha ufugaji ili ubadilike kutoka ufugaji wa kiasili kwenda ufugaji wa kisasa ili kuongeza tija” alifafanua Mhe. Ndaki
Alisema kuwa wafugaji watakaokuwa tayari kubadilisha namna ya ufugaji wao watapelekwa kwenye maeneo hayo yatakayowekewa miundombinu yote muhimu ya ufugaji ikiwemo maji, majani ya malisho na maji.
Wakizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, aliishauri Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuanzisha maeneo ya ufugaji (Runch) kila mkoa na kujenga miundombinu itakayowasaidia wafugaji kufuga mifugo yao kisasa ili waweze kuongeza kipato chao, kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi na kuondokana na umasikini.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Elisante Ole-Gabriel aliiomba Wizara ya Fedha na Mipango kuiwezesha Wizara yake kifedha kwa ajili kufanya utafiti katika sekta ya mifugo ili kuongeza mbinu za kisasa za kuongeza uzalishaji.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Allan Kijazi, alishauri kuwa ili sekta ya mifugo iweze kupiga hatua kubwa, suala la utafutaji masoko kwa ajili ya bidhaa za mifugo, kuongeza elimu kwa wafugaji, pamoja na kuwa na maeneo ya kimkakati ya viwanda vya kuchakata bidhaa za mifugo ni muhimu likafanyiwa kazi.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), kwenye kikao hicho Prof. Elisante Ole-Gabriel, Tanzania ni ya pili kwa kuwa na mifugo mingi barani Afrika kwa kuwa na ng’ombe milioni 33.4, mbuzi milioni 21.29, Kondoo milioni 5.65, Punda 657,380, lakini tija yake bado ni ndogo.
Mwisho.
6 Mei 2021
Home
Unlabelled
Mwigulu Nchemba Ahimiza Ufugaji Wa Kisasa Ili Kusisimua Uchumi Na Maisha Ya Watu