NEWS

6 Mei 2021

Naibu Waziri Ummy: Serikali Kuwapatia Watu Wenye Ulemavu Mafunzo Ya Ujasiriamali

 Na: Mwandishi Wetu - Dodoma
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga amesema kuwa Serikali imejipanga kuendelea kuwapatia Watu wenye Ulemavu mafunzo ya Ujasiriamali ili kuwezesha kundi hilo maalum kujiajiri na kushiriki kikamilifu kwenye shughuli zitakazo wasaidia kujikwamua kiuchumi.

Aliyasema hayo hii leo Mei 6, 2021 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majiliwa (Mb) ambalo liliulizwa na Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Mwantumu Dau Haji, ambaye alitaka kujua ni lini Serikali itaanza kutoa mafunzo ya Ujasiriamali kwa Watu wenye Ulemavu.

Akijibu swali hilo Naibu Waziri Ummy, alieleza kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu imekuwa ikitenga fedha katika kila mwaka wa bajeti kwa ajili ya kuwezesha mafunzo ya ujasiriamali kwa Watu wenye Ulemavu waliopo katika ngazi mbalimbali ikiwemo Halmashauri zote nchini.

“Mafunzo ya Ujasiriamali kupitia Halmashauri yamekuwa yakitolewa kama sharti muhimu wakati wa utoaji wa mikopo itokanayo na asilimia mbili (2%) ya mapato ya ndani ya Halmashauri husika kwa ajili ya kuwezesha Watu wenye Ulemavu kiuchumi,” alieleza Mhe Ummy

Aliongeza kuwa, Serikali imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa watu wenye ulemavu kwenye fani mbalimbali ambazo zimewezesha kundi hilo maalum kuanzisha miradi mbalimbali.

“Kwa mwaka wa fedha 2019/2020 katika Mkoa wa Dar es salaam zaidi ya wajasiriamali wenye ulemavu wapatao 160 walipatiwa mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi wa fedha na uzalishaji wa miradi endelevu,” alieleza Ummy

“Mafunzo hayo yalihusisha Ofisi ya Waziri Mkuu, Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Benki kuu ya Tanzania, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii NSSF, Benki ya Exim, Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu (SHIVYAWATA), Vyama vya Watu wenye Ulemavu na wadau wengine,” alieleza

Sambamba na hayo, alifafanua kuwa Uwezeshaji wa Watu wenye Ulemavu katika mafunzo ya Ujasirimali umekuwa ukiendelea kufanyika kupitia Vyama vyao wakati wa matukio mbalimbali yanayowakutanisha pamoja ikiwemo Mikutano Mikuu ya Vyama vyao pamoja na Maadhimisho mbalimbali ya Watu wenye Ulemavu ambayo hufanyika nchini.