NEWS

21 Juni 2021

Mfumo Wa Mashtaka Ufanane Nchi Nzima – Mpanju


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Amon Mpanju ataka mfumo wa mashtaka nchini uwe unaoeleweka, uliowazi na unaofanana nchi nzima.

Ndg. Mpanju ameyasema hayo leo June 21, 2021 jijini  Arusha wakati akifungua kikao kazi cha wadau kutoka sekta mbalimbali za haki jinai zilizokutana pamoja katika kikao cha siku tatu cha kupata maoni yatakayowezesha kuandaa sera ya taifa ya mashtaka nchini.

“Wadau wote muhimu wamehudhuria kikao hiki na nategemea mtashirikiana kuweka mfumo wa mashtaka unaoeleweka, uliowazi na unaofanana nchi nzima na kuandaliwa kwa sera hii ya taifa ya mashtaka haimaanishi kuwa itaingilia madaraka ya Mkurugenzi wa mashtaka nchini  na kushindwa kufanya majukumu yake” amesema.

Aliongeza kuwa madhumuni ya kukutana katika kikao kazi hicho ni kudadavua, kutoa mawazo na mapendekezo na kupitia sheria zilizowekwa za haki jinai ili kupata sera ya taifa ya haki jinai itakayotuvusha miaka kumi ijayo na kuweka vizuri mfumo wa haki jinai.

Naibu Katibu Mkuu huyo amewataka washiriki hao kushirikiana na kutumia utaalamu wao ili kupata sera inayotakiwa kwani sera hiyo ikikaa sawa haki za binadamu zitalindwa, mfumo wa haki jinai utaeleweka na wananchi watatii sheria.

Pia alisema, sera hii ya taifa ya mashtaka ikikaa vizuri itasaidia mfumo wa mashtaka nchini na maoni yatakayotolewa yatasambazwa kwenye taasisi zote za haki jinai ili kupata sera nzuri zaidi.

Awali akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu huyo kuongea na washiriki wa kikao, Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki Bw. Patience Ntwina amewasisitiza washiriki hao kutoa mawazo yao ili kufanikisha kupatikana kwa sera ya taifa ya mashtaka iliyo bora na itakayosaidia mfumo wa haki jinai.