NEWS

22 Juni 2021

Ofisi Ya Hazina Kufanya Mapitio Na Uchambuzi Wa Kina Wa Mashirika Ya Umma


 Na Mwandishi Maalumu, Arusha
SERIKALI kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina inafanyia kazi dhamira ya kufanya mapitio na uchambuzi wa kina wa mashirika ya umma ili kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan ya kuyafanya yajiendeshe kwa faida.

Kutokana na maelekezo hayo na ili mashirika yaweze kutoa gawio kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Msajili wa Hazina imeandaa kikao kazi chenye lengo la kubadilishana uzoefu wa utendaji kwa lengo la kuongeza tija katika usimamizi na uendeshaji wa biashara katika mashirika hayo.

Alipohutubia Bunge jijini Dodoma, Aprili 22, mwaka huu, Rais Samia alieleza kuwa, “Tunadhamiria pia kufanya mapitio na uchambuzi wa kina kwenye uendeshaji wa mashirika ya umma, tukiwa na lengo la kuyafanya yaweze kujiendesha kwa faida. Mashirika yaliyo mengi yanaendeshwa kwa kusuasua kiasi kwamba unapofika muda wa kutoa gawio la faida serikalini, uongozi na bodi za mashirika wanahaha kunusuru ajira zao.”

Kutokana na hilo, jana jijini Arusha, Ofisi ya Msajili wa Hazina ilizindua kikao kazi cha uandaaji, uchambuzi wa upembuzi yakinifu wa miradi na uchambuzi wa mikopo kulingana na Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada ya Mwaka 1974 na marekebisho yake kwa mashirika ya umma yanayotekeleza miradi mbalimbali ya kisekta na kibiashara.

Akifungua kikao kazi hicho, Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka alisema

licha ya washiriki kubadilishana uzoefu wa utendaji kwa lengo la kuongeza tija katika usimamizi na uendeshaji wa biashara, watapitia na kujadili kwa pamoja miradi mbalimbali inayoweza kujiendesha yenyewe na namna ya kuifadhili kwa kutumia njia mbadala.

Mbuttuka alisema pamoja na jitihada mbalimbali za serikali kwa mashirika ya umma ikiwemo utoaji wa mitaji na kuweka mazingira mazuri ya utoaji wa huduma kwa wananchi, bado mashirika mengi yamekumbwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yake.

Alizitaja baadhi ya changamoto ni ukosefu wa mtaji wa kutosha, utaalamu wa kuandika maandiko ya kibiashara ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo kutoka katika benki na taasisi za fedha na ukosefu wa utaalamu wa kufanya uchambuzi wa mwenendo wa biashara ili kutathimini faida na uendelevu wa biashara kwa kipindi cha muda mfupi na muda mrefu.

“Hali hii kwa kiasi kikubwa imesababisha mashirika mengi kushindwa kujiendesha kwa ufanisi na kulipa gawio kwa serikali,” alieleza Mbuttuka na kubainisha kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia Taasisi, Mashirika ya Umma, Kampuni na Wakala wa Serikali zipatazo 237.

“Kati ya taasisi hizo ni mashirika yapatayo 31 ndiyo yanajiendesha kibiashara. Vile vile, kati ya mashirika hayo ni mashirika yapatayo 12 sawa na asilimia 38.7 yanayojiendesha kwa faida na kulipa gawio kwa serikali wakati mashirika 19 sawa na asilimia 61.3 yanajiendesha kwa hasara na kulipa mchango (CSR) badala ya kulipa gawio kutokana na limbikizo la hasara au hasara zinazotokana na sababu mbalimbali za kiuendeshaji,” alifafanua.

Alisema ili kuongeza ufanisi, ofisi yake imeandaa kikao kazi hicho kwa ajili ya kujengeana uwezo katika maeneo ya uandaaji wa upembuzi yakinifu na matumizi ya Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada katika upatikanaji wa mikopo kwa mashirika ya umma. Yanahudhuriwa na washiriki kutoka katika taasisi na mashirika ya umma.

“Ni matumaini yangu kwamba, kikao kazi hiki kitaleta chachu katika kuboresha utendaji wetu katika kusimamia na kuendesha mashirika yetu yanayofanya biashara na kuhakikisha yanajiendesha kwa faida, kutoa huduma bora kwa jamii na kulipa gawio stahiki kwa serikali,” alisema Msajili wa Hazina.

Alisisitiza kuwa, kutokana na malalamiko kutoka Taasisi na Mashirika ya Umma yanayofanya biashara kwamba washindani wao wa sekta binafsi wanawashinda kwa kuwa ndani ya Serikali kuna urasimu, kikao hicho kitawaleta waandaji wa sera na watekelezaji wake ili pamoja na kujengeana uwezo na kushirikiana namna bora ya kuondoa urasimu kama ikithibitika kuwa upo.

Aliongeza kuwa, ni matarajio yake kwamba kikao kazi hicho kitawezesha washiriki kuwa na uelewa katika uandaaji, uchambuzi na upembuzi yakinifu wa miradi ili miradi itakayokuwa inaibuliwa iwe na vigezo vyote vyinavyokidhi utekelezaji wake vikiwemo kuwezesha kupatikana kwa ufadhili, kuleta manufaa kwa taasisi na kwa jamii na pia kuleta faida.

“Kwa upande wa Taasisi za kifedha, itakuwa ni fursa kuonesha namna mnavyoweza kufadhili miradi na kushirikiana na Mashirika ya Umma katika kuongeza mapato bila kutumia mali za Mashirika zilizopo kama dhamana,” alisema Mbuttuka.