NEWS

22 Juni 2021

Tanzania Mwenyeji Mashindano Ya Mchezo Wa Kabbadi


Mashindano ya Afrika ya mchezo wa Kabaddi kwa mwaka 2021 yanatarajiwa kufanyika hapa nchini  kuanza  Juni  29 hadi 5 Julai, 2021 katika Ukumbi wa Ubungo Plaza Jijini Dar es salaam.

Mchezo huo ambao asili yake ni nchini India umekua ni miongoni mwa michezo inayokuwa hapa nchini kutokana na muingiliano wa mataifa hayo mawili.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul Juni 21, 2021 ametembelea kambi ya timu ya taifa ya mchezo huo katika shule ya Sekondari Nguva wilayani Kigamboni Jijini Dar es Salaam, ambapo amewataka waratibu wa mchezo huo kutoa elimu ili jamii iutambue mchezo huo.

“Natoa rai kwenu kuzishirikisha sekta nyingine katika fursa hii muhimu, mfano sekta ya  Utalii, wanaweza kutumia fursa iliyopo kutangaza vivutio vya Utalii vilivyopo nchini kwa mataifa ambayo yanakuja kushiriki mashindano haya,” amesema Mhe. Gekul.

Aidha, Mhe. Gekul amewataka wachezaji waliopo kambini kufanya mazoezi kwa bidii ili kulibakisha kombe la mashindano hayo  nyumbani, huku akipongeza wadhamini waliojitokeza kudhamini kambi hiyo na kutoa rai kwa wadhamini zaidi kujitokeza.

Mhe. Gekul ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuipa kipaumbele michezo mbalimbali inayofanya vizuri ndani na nje  kwakuwa inasaidia kutangaza nchi, kuibua vipaji pamoja na kuzalisha ajira kwa vijana.

Mashindano hayo yanatarajiwa kushirikisha nchi sita Kenya, Mauritius, Misri, Cameroon  Zimbambwe na wenyeji  Tanzania  ambapo wageni kutoka katika nchi zaidi ya 20 za Afrika wanatarijiwa kuwasili hapa nchini kwa ajili ya kuratibu na kushuhudia mashindano hayo.