NEWS

17 Juni 2021

Waziri Mkuu Atoa Wito Kwa Taasisi Zinazoomba Misamaha Ya Kodi


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa taasisi zinazoomba misamaha ya kodi kwa bidhaa zinazoingizwa nchini zifuate taratibu ikiwa ni pamoja na kueleza kikamilifu ni bidhaa gani wanayotaka kuileta nchini ili ipate msamaha huo na lazima ikidhi matakwa ya Serikali ikiwemo ya kwenda kutoa huduma iliyokusudiwa.

Ametoa wito huo leo (Alhamisi, Juni 17, 2021) wakati akijibu swali la mbunge wa Kilolo Justine Nyamoga katika kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu Bungeni jijini Dodoma. Mbunge huyo alitaka kufahamu Serikali imeweka utaratibu gani wa kutoa misamaha kwa baadhi ya taasisi za dini zinazotoa huduma kwa jamii.

Mbunge huyo amesema taasisi za dini zimekuwa zikikumbwa na urasimu mwingi wakati wa kutoa vifaa au misaada mbalimbali kutoka nje ya nchi hali inayosababisha wakati mwingine vifaa hivyo kukaa muda mrefu bandarini na hatimaye kulazimika kulipia gharama za uhifadhi wakati wanatoa. Alihoji, nini kauli ya Serikali kuhusu tatizo hilo?

Waziri Mkuu amesema Serikali imeweka utaratibu wa kutoa misamaha kwa baadhi ya taasisi zinazotoa huduma za jamii ambazo zinalenga kuisadia katika utoaji wa huduma hizo na taratibu zimeandaliwa vizuri, hivyo wahusika wanapaswa wazifuate ili kuepuka urasimu.

Amesema bidhaa hizo zinavyosafirishwa kutoka nje ya nchi kuingia nchini ili ziweze kupata msamaha wenye bidhaa ambao ni taasisi za dini au nyingine ni lazima wawe wameandaa utaratibu wa kupeleka maombi ofisi husika wakiwa wameambatisha orodha ya bidhaa zilizopo.

”Uzoefu ambao tumeupata Serikalini ni kwamba watu wanaweza kuomba msamaha lakini anachokileta nchini sio kile alichokiombea msamaha, hivyo kunakuwa na hatua ndefu ambazo mwingine husema kwamba hii ni urasimu wa Serikali hapana,”.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali imechukua viwanda vyote ambavyo awali vilikabidhiwa kwa wawekezaji ambao wameshindwa kuviendesha na sasa inafanya uchambuzi kwa ajili ya kuwapa wadau wengine watakaoviendeleza kwa masharti yatakayowekwa.

Ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la mbunge wa Ndanda Cecil Mwambe katika kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu Bungeni jijini Dodoma. Mbunge huyo alitaka kufahamu ni kwa sababu gani viwanda vya korosho havifanyikazi iliyokusudiwa.

(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,