NEWS

23 Septemba 2014

Diamond Platnumz yamkuta makubwa Uingereza, atapeliwa, Polisi wamsaka

Ni nuksi, gundu au hujuma? Ndivyo unavyoweza kujiuliza kufuatia tukio lingine baya lililomkuta staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ akiwa London nchini Uingereza ikiwa ni siku kadhaa tangu aliposababisha vurugu nchini Ujerumani, Ijumaa Wikienda lina ripoti kamili ya kilichojiri.





TWENDE LONDON
Habari kutoka kwa ‘mtu wetu’ aliyeko jijini London zilieleza kwamba Ijumaa iliyopita Diamond alitarajiwa kufanya shoo kubwa kwenye Ukumbi wa LaFace jijini humo lakini mambo yakamwendea kombo na kujikuta akihenyeshwa na polisi kwa kushindwa kufanya shoo hiyo iliyokuwa imetangazwa kupita maelezo.

‘ACHAFUA’ KURASA ZAKE
Kwa siku mbili mfululizo, Diamond alichafua kurasa zake za mitandao ya kijamii kwa kuweka mabango na kuitangaza shoo hiyo kwa fujo za kufa mtu.

DIAMOND AALIKA WATU, AOMBA ACHAGULIWE LISTI YA NYIMBO
Saa kadhaa kabla ya shoo, Diamond alitumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kuwaalika watu kwenye shoo hiyo kubwa huku akiomba wampatie listi ya nyimbo wanazotaka awaimbie, jambo ambalo mashabiki wake walilifanya.



Promota wa Diamond wa UK 

UKUMBINI
Ilielezwa kwamba usiku ulipoingia watu walianza kumiminika ukumbini.

TUKIO
“Unaambiwa watu walisubiri mpaka usiku wa manane hawamuoni Diamond.
“Baadhi ya mashabiki walianza kupiga kelele ndipo uongozi wa ukumbi huo ukawaambia hata wao walikuwa hawajalipwa fedha za ukumbi.

“Ilipofika alfajiri, baadhi ya mashabiki walitaka kufanya fujo ndipo uongozi wa ukumbi ukaamua kuwarudishia viingilio vyao kwa sababu Diamond alifuatwa hotelini, akagoma kwenda ukumbini hadi alipwe chake kwanza,” kilisema chanzo chetu kilichohudhuria ukumbini humo.

TOFAUTI NA UJERUMANI
Tofauti na Stuttgurt, Ujerumani ambako mashabiki walifanya uharibifu mkubwa, mashabiki wa London waliamua kuwa wapole tu na kurejea majumbani mwao na hasira walizozimeza vifuani huku polisi wakifanya kazi ya ziada kutuliza ghasia.




DIAMOND MIKONONI MWA POLISI
Baada ya upepo kutulia, ilisemekana kwamba polisi walimfuata Diamond hotelini na kumpeleka kituoni ambako alitoa maelezo yake.
Ilielezwa kwamba Diamond aliwaambia polisi kuwa promota alishindwa kumlipa fedha yake hivyo asingeweza kufanya shoo ya bure.

DIAMOND MITANDAONI
Diamond alimtupia lawama promota huyo ambapo mara tu baada ya kutoka kituoni aliandika kwenye kurasa zake za kijamii:
“Tafadhali ndugu zangu wa UK (Uingereza)!!!….kuweni makini sana na promota huyu (Victor – Dj Rule) mnaposikia kaandaa shoo, party au hafla yoyote…ni vyema kuziepuka na kutohudhuria kabisa kwa sababu ni tapeli…. si unajua aisifiae mvua imemnyeshea… basi mie nimeloa kabisa.”




DIAMOND ATAFUTWA
Baada ya kunyetishiwa mkanda mzima, Jumamosi iliyopita, Ijumaa Wikienda lilimtafuta Diamond ambapo alipopatikana alikuwa tayari ametua nchini Ujerumani kwa ajili ya ile shoo ya bure aliyotakiwa kuifanya ili kulipiza ile iliyoharibika.
Staa huyo alikiri kukutwa na mkasa huo na kuwatahadharisha wasanii wengine wa Bongo kuwa makini:
“Jamani kama ni kuniabisha, kweli wameniaibisha lakini ndiyo kwanza napata mzuka wa kufanya kazi kwa bidii.”

BABU TALE ANASEMAJE?
Kutoka kwa Diamond, gazeti hili lilimgeukia meneja wake, Babu Tale ambaye hakuambatana na Diamond akakiri kuwa ishu kama hizo zinawaharibia sana.

MPANGO WA KUMMALIZA?
Kwa mujibu wa wadau waliokuwa na maswali mengi bila majibu hasa ishu ya kuwepo kwa mkataba, kuna mpango wa kummaliza Diamond kimataifa hasa barani Ulaya kwani ameshakwenda Marekani mara nyingi na kufanya shoo nyingi bila matatizo kama hayo.