NEWS

23 Septemba 2014

Jack Patrick aiukumbuka Tanzania, Huu ndio ujumbe wake kwa watanzania




MWANAMITINDO wa Bongo aliyepo nyuma ya nondo huko Macau, Hong Kong nchini China akitumikia kifungo cha miaka sita baada ya kukutwa na hatia ya kubeba madawa ya kulevya ‘unga’, Jacqueline Fitzpatrick Cliff ‘Jack Patrick’ ametuma ujumbe mzito kwa mashabiki wake.




Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili, rafiki wa karibu wa Jack ambaye hakupenda jina lichorwe gazetini, alisema kwamba mwanamitindo huyo amekuwa akimuandikia barua mara kwa mara lakini safari hii ametaka ujumbe wake uwafikie Watanzania.

“Amesema watu wasimhurumie kuhusu kufungwa, amesisitiza sana juu ya suala mavazi na mitindo. Amesema hapendi kuona Tanzania inayumba katika masuala ya mitindo ambayo yeye alikuwa akiiamini kwamba ni kazi ambayo inaweza kuwaingizia kipato watu wengi,” alisema rafiki huyo wa karibu.




Mwanamitindo wa Bongo, Jacqueline Fitzpatrick Cliff ‘Jack Patrick’ akiwa chini ya ulinzi China.

Rafiki huyo alizidi kuweka wazi kuwa mara nyingi Jack hapendi kuwaambia juu ya maisha ya jela kwani hapendi kabisa kuwapa watu simanzi bali anapenda watu wajue anaishi maisha ya kawaida.
“Mara nyingi Jack hapendi kabisa kueleza maisha ya jela, hapendi kuwaumiza wat, anachopenda ni kujua nini kinachoendelea katika fasheni,” alisema rafiki huyo wa Jack.

Rafiki huyo alisema kuwa Jack bado anaagiza nguo ambazo alikuwa akipenda kuvaa hasa lineni nyeupe na kuwataka watu wahisi kama yupo masomoni na atarejea tu akiwa salama.
Jack alikamatwa Desemba 19, mwaka jana akiwa amebeba madawa ya kulevya aina ya Heroin yenye uzito wa kilo 1.1 katika Uwanja wa Ndege wa Macau akitokea Bangkok, Thailand kuelekea Guangzhou, China.