NEWS

9 Septemba 2014

Ni ugaidi asilimia 100 , kwa waliyofanyiwa askari hawa

TUKIO la kutisha la kushambuliwa kwa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, ambapo askari wawili walipoteza maisha na silaha kadhaa kuporwa, limeelezwa kuwa kwa kiwango cha asilimia mia moja, jambo hilo ni ugaidi wa dhahiri.

Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, kilichoshambuliwa kwa mabomu.

Jumamosi iliyopita, majira ya saa sita usiku, watu wasiojulikana, walikivamia kituo hicho kwa mabomu na silaha zingine nzito zinazosadikika kuwa ni za kivita, wakafanya mauaji na kujeruhi watu wengine kadhaa kabla ya kupora bunduki na silaha zilizohifadhiwa kituoni hapo.


Damu ya maaskari iliyomwagika kwenye shambulia hilo la kigaidi.

“Huu siyo ujambazi wa kawaida uliozoeleka, ni kweli kuna wakati matukio yanatokea kuwa ya kutisha sana, lakini aina hii ya mashambulio siyo kawaida, tena kituo cha polisi? Hawa watu ni dhahiri walihitaji kupata silaha tu, sasa sijui zinakwenda kutumika wapi na tuna shaka kama hawa si Watanzania,” alisema Zebareta Shayo, mkazi wa Sinza, jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi wa Mashtaka (DCI) Isaya Mngulu.

Taarifa kutoka eneo la tukio zinasema kuwa baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, (IGP) Ernest Mangu na Mkurugenzi wa Mashtaka (DCI) Isaya Mngulu kuwasili tangu juzi mkoani hapa, askari zaidi kutoka Mikoa ya Tabora, Shinganya na Mwanza wanaendelea kuwasili.

Msako mkali unaendeshwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kuweza kuwabaini wahalifu hao huku Kamanda wa Mkoa wa Geita, Joseph Konyo akiwataka wananchi kutoa taarifa mara moja watakapotilia shaka nyendo za mtu yeyote ili kurahisisha zoezi hilo alilodai lazima lifanikiwe.

Juni 10, mwaka huu, tukio kama hilo likihusisha majambazi waliokisiwa kuwa sita, wakiwa na pikipiki tatu walivamia Kituo Kidogo cha Polisi Mkamba kilichopo Kimanzichana, Wilaya ya Mkuranga, Pwani na kuua askari mmoja na mgambo na kujeruhi mgambo mwingine kisha kupora bunduki tano na risasi 60.


Waziri Salum, mwanasheria na wakili wa kujitegemea alisema tukio hilo ni vizuri kama lingeifanya serikali kutazama upya mipaka yetu kwani kuna kila dalili kuna baadhi ya wageni wanaingia kirahisi na kufanya unyama huo bila kujulikana.

Mfano wa silaha zilizoibwa na majambazi.

Askari waliopoteza maisha katika shambulio hilo wametajwa kuwa ni Uria Mwandiga mwenye namba WP 7106 na Dustan Kimati mwenye namba G 615 PC. Majeruhi ni David Ngupama Mwalugelwa (44) namba E 5831 APL na Mohamed Hassan Kilomo (25) namba H 627 PC.