Akitoa matokeo ya awali ya utafiti huo, mmoja wa watafiti wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili, kitengo cha magonjwa na afya ya akili, Lusajo Kajula, alisema kuwa asilimia 10 ya vijana wenye umri wa miaka 12 hadi 14 ambao ni wanafunzi wa darasa la tano na sita wameshawahi kufanya ngono.
Alisema ngono hiyo kwa asilimia kubwa hufanywa na wanafunzi hao kinyume na maumbile.
Kajula alisema vijana wengi wamebainika kufanya ngono ya kawaida na ya mdomo, ikifuatiwa na ngono ya kinyume na maumbile.
Alisema kwa wale ambao wameshawahi kufanya ngono, asilimia 6.3 wamefanya kinyume na maumbile wakati asilimia 93.7 hawajawahi kufanya.
Alisema utumiaji wa kondomu umebainika kuwa mdogo kwa vijana wadogo ambao wameanza kufanya ngono.
“Asilimia 68 ya wale walioanza kufanya ngono hawajawahi kutumia kondomu kabisa, wakati asilimia 32 wamewahi kutumia,” alisema.
Alisema hiyo ni sehemu ya utafiti wa miaka minne ulioshirikisha Chuo Kikuu cha Makerere cha Uganda, Cape Town na Limpopo vya Afrika Kusini, Bergen na Oslo vya Norway, Maastricht cha Uholanzi na Sussex cha Uingereza.