NEWS

21 Machi 2017

Siri Muhimu Unazotakiwa Kuzijua Kuhusu Wanawake...!!!


Wanawake wana siri nyingi sana mioyoni mwao na kwa kawaida huwa hawawezi kuonesha hisia zao za ndani moja kwa moja. Ni watu ambao mara nyingi hupenda kuwasilisha vilivyomo ndani yao kwa ishara.

 Kwa mtindo wa maisha ya wanaume wengi wa sasa ni vigumu kusoma ishara hizo na kujua mahitaji ya mwanamke husika. Bahati mbaya ni kwamba, ukienda kinyume na mahitaji yao, utashangaa kila siku mnaingia kwenye mikwaruzano isiyo na msingi.

Wiki iliyopita nilieleza machache, leo tunaingia katika sehemu ya mwisho. Hebu fuatilia kwa makini ujue mwanamke anapenda vitu gani hasa ili uweze kuishi naye kwa amani.

KUSIKILIZWA

Ukitaka kumpatia mwanamke, msikilize. Kumbuka wanawake wengi wana hulka ya kuongea sana! Ndivyo walivyo.

Wakati fulani, mwanamke anapenda kuzungumza mambo fulani na mwanaume wake.

Pengine anapenda kumshauri au kujadiliana naye jambo fulani; huenda ana mawazo mazuri lakini mtindo wao wa kuongea sana unaweza kukatisha tamaa. Usifanye hivyo. Mpe nafasi.

Msikilize kwa makini, mwishowe unaweza kupata manufaa makubwa kutokana na maneno yake. Amini usiamini, hata katika mambo yanayohusu mafanikio, ukimshirikisha mkeo, huwa na mawazo mazuri yanayochochea kuifukuzia ndoto yako.

Ukiachana na hilo, mwanamke anaweza kukuambia, hapendi mavazi yako – hapendi nguo fulani unayovaa, labda kwa hoja kuwa haikupendezi! Usimdharau. Sikiliza hisia zake.

Kumbuka upo kwa ajili yake, anaweza kujiuliza, kama anakuambia mavazi hayo si mazuri kulingana na umbo lako na ung’ang’ania, unamvalia nani huko nje? Msomaji mmoja aliwahi kuniambia: “Yaani kaka Shaluwa, mume wangu ananishangaza sana.

“Anapenda kuvaa suruali za vitambaa, pana na mashati makubwa kama Mzaire. Nimeshamwambia mara nyingi kuwa sipendi na hapendezi, lakini bado analazimisha kuvaa. Ananinyima raha sana, maana hata nikiongozana naye, nakuwa kama nipo na mtu mzima!”

Unaweza kuona namna gani wanawake wanavyokereka na mambo madogo tu lakini wakiyapa uzito 
wa hali ya juu.

MSIMAMO

Wanawake wanapenda mwanaume mwenye kujiamini na kusimamia msimamo wake. Unaweza kushangaa lakini wakati mwingine mwanamke anaweza hata kukuweka kwenye mtego; mnakubaliana jambo lakini baadaye anajifanya kukupinga ili kuona msimamo wako.

Wanaamini katika mwanaume anayejielewa na asiyeyumba wala kuyumbishwa. Kwamba, mwanaume wa aina hiyo ni rahisi kufikia ndoto za familia – yeye kama kiongozi wa nyumba.

ZAWADI

Si lazima ununue gari jipya na kumpelekea kama zawadi. Kumchagulia wimbo mzuri redioni, kadi yenye mashairi mazuri ya kimapenzi, bangili, vipodozi na vitu vingine vidogovidogo huwafurahisha sana wanawake.

MTOKO

Hata kama ni mara moja baada ya miezi miwili, ukitoka na mwenzako na kwenda naye kupata chakula cha jioni mgahawani huongeza mapenzi. Kwa mwanamke ni jambo kubwa lenye thamani sana.