WiKi iliopita, Tanzania tulibarikiwa kwa kupokea ugeni mzito wa viongozi wa juu kabisa wa soka ulimwenguni ambapo Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Gianni Infantino alitua hapa nchini. Infantino hakuja peke yake, bali aliongozana na viongozi wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) chini ya rais wake Ahmad Ahmad ambapo walikuja kuhudhuria mkutano wa siku mbili kujadili masuala mbalimbali ya soka, hasa la vijana na wanawake.
Wakati Infantino anakanyaga ardhi yetu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, aliulizwa ni mwanasoka gani ambaye anamjua kutokea hapa nchini. Rais hiyo hakusita kulitaja jina la nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Samatta kama mchezaji ambaye anamfahamu kwa sababu ya kucheza soka Ulaya ndani ya nchi ya Ubelgiji.
Kitendo cha Infantino kumtaja mchezaji mmoja tu wa hapa nchini kuwa ndiye anayemfahamu ina maana kwamba Samatta ameweza kuipeperusha bendera ya taifa kwa ufasaha kabisa kwani kufahamika na kiongozi mkubwa kama yule ni jambo zuri kwetu.
Pia kimetupa mwanga kwamba kama wachezaji wengine ambao wamejazana hapa Bongo wakifanya jitihada za kwenda kucheza soka Ulaya basi tunaweza kupiga hatua kutoka tulipo na kufika katika nchi ya ahadi. Naamini huu ndiyo muda sasa kwa wachezaji kuiga mfano wa Samatta na wao waweze kutoka na kwenda kucheza nje kwani ukitazama tuna utitiri wa wachezaji wenye vipaji.
Nje ya suala la mkutano huo, ligi yetu na kombe la FA ziliweza kuendelea katika viwanja mbalimbali mara baada ya ugeni kuondoka nchini na tunaamini mkutano ule ulikuwa na faida kubwa kwetu. Tumeona katika Kombe la FA, timu zikifanikiwa kutinga hatua ya robo fainali baada ya kushinda mechi zao licha ya nyingine huenda hazikupewa nafasi ya kufanya hivyo kwa kuwa kwenye ligi zimekuwa zikionyesha kiwango cha kawaida.
Hapa ninachotaka kukisema ni kwamba katika kombe hili, mpaka sasa hivi kwa timu zote ambazo zimefanikiwa kutinga hatua hiyo, hakuna mwenye uhakika wa kuweza kutwaa ubingwa ambao ndiyo unatoa tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa, hivyo kila timu ina nafasi ya kuweza kutwaa ubingwa huo iwapo itaendelea kupambana. Lakini kuna baadhi ya mechi za ligi pia zimeweza kupigwa na tumeshuhudia matokeo ya kushangaza katika baadhi ya mechi ambayo huenda hayakutarajiwa kutokana na aina ya timu ambazo waliweza kucheza nazo.
Tumeona vinara wa ligi Simba wakipata matokeo makubwa dhidi ya timu ambayo inasifika kuwa ni ngumu Mbao, hapa nataka niseme kwamba mchezo huu umetuonyesha kwamba ligi yetu ni mtindo gani kwa kuwa tumekuwa tukicheza kwa kukamiana. Mbao tangu wapande wamekuwa na rekodi nzuri na hizi timu kubwa lakini inapokuwa inacheza na timu za saizi yao hupotea kabisa kitu kinachoonyesha kwamba asilimia kubwa ya timu nyingi wao wanafikiria kuzikamia Simba na Yanga jambo ambalo haliwezi kuleta ushindani wa ukweli.
Ligi haiwezi kuwa bora kama hizi timu ndogo zitaendelea kuzikazia Simba, Yanga na Azam pekee halafu wakikutana wenyewe kwa wenyewe wanacheza kawaida, lazima wabadilike na ndiyo maana Mbao wao waliweza kupata kipigo cha aibu kutokana na rekodi yao.
Mwisho niendelee kusisitiza kwa timu ambazo zinashiriki michuano ya kimataifa kufanya maandalizi ya uhakika kabla ya mechi zao za raundi ya kwanza, Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Simba katika Kombe la Shirikisho, kwa kuwa ndiyo ugumu na fitina za mashindano hayo. Huu si wakati wao kushangilia matokeo ya ligi kwa kuwa mashabiki kiu yao ipo katika michuano hiyo kwa kuwa wanataka kuona timu zikifika mbali na siyo kila msimu kuishia katika hatua za mwanzo au makundi, kitu ambacho kwa wapenzi wa mpira kinawakera na hawapaswi kubweteka.
Na Mohammed Hussein, 18 za chinga one mawasiliano +255 789 343 414 mohammedhussein@yahoo.com
The post Kidogo Heshima ya Ligi Inarejea, Simba, Yanga Wasibweteke appeared first on Global Publishers.