NEWS

28 Februari 2018

Ngassa Atafuta Sifa Kwa Yanga SC Nangwanda

 

KIKOSI cha timu ya Yanga, leo Jumatano kinapambana kufa au kupona kuhakikisha kinavunja rekodi yake mbaya kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona kitakapopambana na Ndanda.

 

Tangu msimu wa 2014/15, ambao Ndanda walipanda daraja, kwenye Ligi Kuu Bara Yanga imecheza uwanjani hapo mechi mbili na zote imetoka uwanjani bila ya kufunga bao jambo ambalo leo linaweza kuwa mwisho au kama Yanga wakizembea likaendelea. Mechi ya kwanza msimu huo, Yanga na Ndanda zilitoka suluhu kwenye Uwanja wa Taifa, kisha zilipokwenda Nangwanda Ndanda ikashinda kwa bao 1-0.

 

Msimu uliofuatia wa 2015/16, Yanga ilishinda bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, kisha mechi ya pili zilitoka sare ya kufungana mabao 2-2. Mchezo huo wa pili ulichezwa tena Uwanja wa Taifa badala ya Nangwanda kutokana na makubaliano maalum. Msimu uliopita, katika Uwanja wa Nangwanda, timu hizo hazikufungana, lakini zilipocheza Uwanja wa Taifa, Yanga ilishinda mabao 4-0.

 

Msimu huu, mechi ya kwanza Uwanja wa Uhuru, Yanga ilishinda 1-0. Ofisa Habari wa Ndanda, Idrisa Bandari, amesema kuwa: “Vijana wetu wapo tayari kwa mchezo huo, tunataka kushinda ili kumaliza vizuri ligi msimu huu. Yanga ni timu kubwa, tunaiheshimu, lakini tunahitaji kuendeleza rekodi yetu dhidi yao katika uwanja wetu wa nyumbani.” Naye Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten, alisema:

 

“Kiujumla maandalizi yamefanyika vya kutosha na vijana wapo tayari kwa mchezo, nimezungumza na Kocha Mkuu George Lwandamina, amesema kinachotakiwa ni ushindi tu bila ya kujali yaliyopita, lengo likiwa ni kujitengenezea nafasi nzuri ya kuwania ubingwa.” Ngassa atafuta sifa Ngassa ni moja kati ya wachezaji walioitumikia Yanga kwa mafanikio makubwa kipindi cha nyuma na leo atakutana nao kwa mara ya kwanza baada ya kusajiliwa kwenye dirisha dogo na Ndanda FC na amefunga bao moja tu tangu asajiliwe.

 

Ameiambia Championi Jumatano kuwa; “Tunahitaji matokeo mazuri na binafsi nahitaji kulinda heshima yangu na ya watu wa Mtwara waje kwa uwingi kuona kile ambacho tutawapa wapinzani wetu watanisamehe kwa hilo.” “Na ukizingatia wananchi wa Mtwara wamenipa zawadi toka nifikie hapa na hivyo ninaamini kesho nikijituma kwa bidii nitafanya mambo mazuri ambayo yataibeba timu yangu,” alisema mshambuliaji huyo.

The post Ngassa Atafuta Sifa Kwa Yanga SC Nangwanda appeared first on Global Publishers.