Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemsomea maelezo ya awali mkurugenzi mkuu wa zamani wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando anayekabiliwa na mashtaka matano likiwamo la matumizi mabaya ya madaraka.
Kabla ya kusomewa maelezo leo Februari 28,2018 mbele ya Hakimu Mfawidhi, Victoria Nongwa, Wakili wa Serikali Dismas Mganyizi, alimkumbusha mashtaka yanayomkabili Tido anayetetewa na wakili Ramadhani Maleta.
Baada ya kusomewa, Tido ambaye yuko nje kwa dhamana amekubali maelezo binafsi na kwamba alikuwa mkurugenzi mkuu wa TBC mwaka 2006 hadi 2010.
Amekubali kuwa alikuwa msimamizi wa shughuli za TBC lakini si zote.
Pia amekubali kutoa maelezo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kuwa alifikishwa mahakamani Januari 26,2018.
Tido amekana mashtaka yanayomkabili na upande wa mashtaka katika kesi hiyo utaanza kutoa ushahidi Machi 28,2018.
Anakabiliwa na mashtaka manne ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh887.1 milioni.
Tido anadaiwa Juni 16,2008 akiwa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), akiwa mkurugenzi mkuu wa TBC kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kuendesha na kutangaza vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila kupitisha zabuni kinyume cha sheria ya ununuzi, hivyo kuinufaisha BVl.
Katika shtaka la pili anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake ikielezwa Juni 20,2008 alisaini makubaliano ya utangazaji wa digitali duniani kati ya TBC na BVl.
Tido katika shtaka la tatu anadaiwa Agosti 11,2008 na Septemba 2008 akiwa Dubai alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano ya ununuzi, usambazaji, kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na kuifaidisha BVI.
Shtaka la nne, anadaiwa Novemba 16,2008 akiwa Dubai alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano ya kuendesha miundombinu ya utangazaji kati ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI.
Tido katika shtaka la tano anadaiwa kati ya Juni 16 na Novemba 16,2008 akiwa Dubai aliisababishia TBC hasara ya Sh887.1 milioni.