NEWS

20 Februari 2018

Ratiba Kuagwa Mwili wa Akwilina Dar

 

BAADA ya maridhiano ya kuuchukua mwili katika Hospitali ya Taifa Mhimbili, familia ya aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline aliyeuawa kwa kupigwa risasi imetoa ratiba ya kuagwa kwa mwili w binti huyo.

 

Akizungumza baada ya kupokea ripoti ya mwili wa marehemu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kaka wa marehemu, Moi Kiyeyeu alisema kuwa mdogo wake ataagwa Alhamisi hii Februari 22, katika viwanja vya Chuo cha NIT kilichopo Mabibo jijini Dar na baadaye atasafirishwa kwenda nyumbani kwao Rombo-Mashati mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi.

 

Kwa mujibu wa ndugu wa marehemu, ripoti ya uchunguzi waliyopewa na madaktari wa Muhimbili inaonesha kuwa marehemu alipigwa risasi kichwani iliyoingia upande wa kushoto na  kutokea upande wa kulia.

 

“Ripoti tuliyopewa inaonesha kichwa cha marehemu kilipasuliwa na risasi ambayo iliingia upande wa kushoto na kutokea upande wa kulia ambao umefumuliwa vibaya,” shemeji wa Akwilina, Festo Kavishe alisema.

 

Akwilina alifariki dunia Februari 16, 2018 baada ya kupigwa risasi kichwani akiwa kwenye daladala wakati polisi wakiwatawanya waandamanaji ambao ni wafuasi wa Chadema.
Polisi Dar inawashikilia watu 40 na askari sita kufuatia tukio hilo ambapo Kamanda Mambosasa amesema wameunda timu ya upelelezi ili kuchunguza chanzo cha kifo hicho.

The post Ratiba Kuagwa Mwili wa Akwilina Dar appeared first on Global Publishers.