Msemaji wa Mabingwa Watetezi, Klabu ya Simba, Haji Manara amehoji Mamlaka ya mapato Tanzania juu utaratibu wa watani zao wa jadi kuhusu kuchangisha kwa ajili ya klabu yao na kuuliza kama utaratibu huo ni sahihi.
Manara amehoji iwapo kama Klabu hiyo inayoongoza msimamo wa ligi kuu soka Tanzania bara kama inalipia kodi katika Mamlaka hiyo huku akisistiza kwamba hata kama ukweli ukiwa mchungu kiasi gani lazima usemwe.
"TRA nakumbuka mlienda katika kanisa la Mchungaji Kakobe kufuatilia ile michango na zile sadaka za waumini, Vipi kwa hawa wanaochangisha kila uchwao? wana mashine za EFD? wanalipia kodi za hizi Rambirambi za kujitakia?", ameandika Manara.
Katika kusisitiza kauli yake, Manara amesema "Nategemea 'soon' (mapema) wahusika watatoa maelekezo sahihi ya huu utamaduni unaotufedhehesha Watanzania na ambao ukiachwa unaweza kusababisha kizungumkuti cha kukokotoa hesabu".