NEWS

31 Desemba 2018

Rekodi ya Makambo Yaitesa Simba

MAMBO ni moto! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya mshambuliaji wa Yanga, raia wa DR Congo, Heritier Makambo, kuandika rekodi ya pekee hivi karibuni katika michuano ya Ligi Kuu Bara ambayo ilimshinda mshambuliaji wa kimataifa wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi msimu uliopita.

 

Rekodi hiyo si nyingine bali ni ile ya kupachika mabao mengi katika mechi za mikoani ambazo Yanga imecheza mpaka sasa dhidi ya Mwadui FC, Kagera Sugar, Prisons, African Lyon pamoja na Mbeya City. Katika mechi hizo, Yanga imefanikiwa kushinda zote huku ikijipatia mabao 10 ya kufunga lakini pia ikifungwa manne.

 

Katika mechi dhidi ya Mwadui FC ilishinda 2-1, ikaichapa Kagera Sugar 2-1, ikaifunga Prisons 3-1, kisha ikaichapa 1-0 Afican Lyon na juzi Jumamosi kifanya tena hivyo dhidi ya Mbeya City kwa kuifunga mabao 2-1.

Katika mabao hayo 10 ambayo Yanga imefunga mikoani, manne kati ya hayo yamefungwa na Makambo na kufanikiwa kuandika rekodi ya pekee ambayo msimu uliopita licha ya Okwi kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akiwa amefunga mabao 20, alishindwa kuiandika rekodi hiyo. Katika mechi 12 za msimu huo uliopita wa 2017/18 ambazo Simba ilicheza mikoani Okwi alifanikiwa kufunga mabao mawili tu kati ya 20 iliyofunga msimu huo.

 

Mabao hayo alifunga dhidi ya Mwadui FC kwenye Uwanja Kambarage, mijini Shinyanga pamoja na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro. Kutokana na hali hiyo, Makambo ameonyesha kuwa ni moto wa kuotea mbali katika viwanja vya mikoani kushinda Okwi ambaye pia msimu huu katika mechi nne za mikoani ambazo ameitumikia Simba amefanikiwa kufunga bao moja tu ambalo alilifunga dhidi ya Mwadui FC katika mchezo ambao Simba ilishinda kwa mabao 3-1.

 

Akizungumzia hali hiyo, Makambo ameliambia Championi Jumatatu kuwa: “Nashukuru Mungu kwa rekodi hiyo ila bado sijatosheka, nataka kufunga katika kila mechi nitakayocheza. “Naomba Mungu anijalie afya njema niwe fiti niweze kutimiza lengo langu hilo.”

 

Akiizungumzia kasi hiyo ya upachikaji mabao kwenye viwanja vya mkoani, kiungo mkabaji wa Simba, Jonas Mkude alisema: “Makambo ni mchezaji mzuri, lakini pia rekodi yake katika viwanja hivyo siyo mbaya, ni nzuri, kwa hiyo nimpongeze tu kwa hilo.” Mpaka sasa katika michuano ya Ligi Kuu Bara msimu huu, Makambo ndiye anayeongoza kwa kuzifumania nyavu akiwa na mabao 11, wakati Okwi yeye anashika nafasi ya nne akiwa na mabao saba.

SWEETBERT LUKONGE, Dar es Salaam

The post Rekodi ya Makambo Yaitesa Simba appeared first on Global Publishers.