NEWS

2 Januari 2019

Bei ya Petrol, Dizel na Mafuta ya Taa nchini Yashuka

Bei ya mafuta nchini imeshuka kwa kati ya Sh140 hadi zaidi ya Sh230 kwa lita moja katika maeneo mengi.

Taarifa ya kila mwezi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), inaonyesha unafuu huo kwa watumiaji wa petroli, dizeli na mafuta ya taa.

Pia yale yanayouzwa bei ya jumla yameshuka kwa viwango karibu na ya rejareja.

Taarifa iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Ewura, Nzinyangwa Mchany inaonyesha kuwa kuanzia leo, bei ya rejareja ya petroli imeshuka kwa Sh141 wakati ile ya dizeli ikipungua kwa Sh212 na mafuta ya taa Sh167 kwa kila lita. Bei hizo ni kwa mafuta yanayopitia Bandari ya Dar es Salaam.

Hali ikiwa hivyo kwa mafuta yanayopitia Dar es Salaam, Bandari ya Tanga na ukanda wa kaskazini kwa ujumla nao bei ya rejareja ya petroli imepungua kwa Sh237 na ile ya dizeli kwa Sh138 wakati ya mafuta ya taa yakipanda kwa Sh4.

Mwezi uliopita hakuna mzigo ulioshushwa katika Bandari ya Mtwara inayohudumia mikoa ya kusini ya Lindi, Mtwara na Ruvuma itakayolazimika kuagiza nishati hiyo kutoka jijini Dar es Salaam.

Bei ya mafuta kwenye mikoa hiyo, ripoti ya Ewura inasema itakuwa sawa na Dar es Salaam ukijumlisha na gharama za usafirishaji.

Kuhusu kutotumika kwa Bandari ya Mtwara, Msemaji wa Ewura, Titus Kaguo alisema hakuna mfanyabiashara aliyepitishia mafuta yake katika bandari hiyo na mamlaka hiyo haina uwezo wa kuwalazimisha waagizaji waitumie.

Mamlaka hiyo imevitaka vituo vyote vya mafuta kubandika bei za bidhaa wanazouza sehemu ya wazi ili kila mtu aweze kuziona huku ikiwakumbusha wateja kupiga *152*00# kujua bei ya mahali walipo.