NEWS

2 Januari 2019

UVCCM Wataka Muungano Wetu Ulindwe

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umetoa mwito kwa Rais John Magufuli na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, kuhakikisha hakuna chokochoko dhidi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
 
Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa,
Tabia Mwita, wilayani Tarime, Mara kwenye kikao cha Baraza Kuu la umoja huo wilayani hapa.
 
Amesema waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Aman Karume, wanapaswa kuenziwa kwa kuulinda muungano. Amesema amani ya nchi ndiyo daraja la maendeleo.
 
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania uliasisiwa Aprili 26, 1964.
 
Mwita amesema migogoro sharti ipatiwe suluhu. “Mfano, hapa Tarime kuna migogoro mingi ya ardhi…viongozi wa serikali wapo, lakini haiishi. Sasa nakwenda kumwambia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,” amesema.
 
Kuhusu ajira, amesema ni kilio cha dunia nzima. “Shirika la Kazi Duniani (ILO), limesema changamoto ya ajira ni ya dunia nzima. Kazi na ajira ni vitu viwili tofauti. 

Kazi maana yake mtu anafanya kazi yoyote bila kujali ameajiriwa ili kujipatia kipato. Ajira ni mtu anayesubiri aajiriwe ndipo afanye kazi,” amesema.
 
Amewataka vijana na wananchi kwa jumla kuongeza juhudi katika kufanya kazi badala ya kusubiri ajira.
 
Amesema wakati viongozi wakuu wa serikali wakipambana kukuza uchumi, vijana wana wajibu kuhakikisha chama hicho kinashinda uchaguzi, akisema ushindi ni lazima. 

Kuhusu kahawa, amesema: “Nimeambiwa hapa Tarime mnalima pia kahawa. Hatutaki ikauzwe na kutengenezwa nje ya nchi halafu irudi kuuzwa kwa bei ya juu. Izalishwe na kutengenezwa hapa hapa,” amesema Mwita.
 
Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Tarime, Godfrey Francis, amesema wanajiandaa kuingiza basi litakalokuwa kitega uchumi cha umoja huo.
 
“Pia tunatafuta mbia atujengee jengo la kitega uchumi la ghorofa tano hapa Tarime. Hatutaki mchezo,” alisema Francis na kuongeza;
 
“Lakini ni fursa wenyeviti wa vijana na viongozi wote, mtu yeyote anayemkosoa vibaya Mwenyekiti wetu wa CCM Taifa, mimi nafikiri hakuna haja ya kupeleka kesi polisi. Sisi tupige, wao ndio wakashtaki wenyewe.
 
“Ndiyo kazi kubwa sisi tunayo. Kama kiongozi wetu anadhalilishwa sisi tupo viongozi tunamuangalia tu, maana yake sisi pia tunamuunga huyo mkono.”
 
Kikao hicho kilihudhuriwa na Mbunge wa Viti Maalumu ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Agnes Marwa.
 
Wengine ni Katibu wa UVCCM Mkoa wa Mara, Hassan Moshi, Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Musoma, Emmanuel Nestory, Mhasibu mstaafu wa CCM Tarime, John Gimunta, na viongozi wengine kadhaa.