Kama uliona picha za hivi karibuni za staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Rais Mstaafu wa Tanzania wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Mrisho Kikwete ‘JK’ ambazo zilizua gumzo bila kujua ni nini kilikuwa kinaendelea, basi Risasi Mchanganyiko linakujuza.
JK AMWITA MONDI Taarifa ikufikie kwamba, JK alimwita Diamond au Mondi nyumbani kwake jijini Dar na kumpa wosia mzito ambao uligeuka gumzo huku staa huyo akikomaliwa juu ya mambo matatu ndani yake.
Wapo baadhi ya wadau waliodhani kuwa Diamond alikwenda kumuomba JK amsaidie kwenye ule msala wake na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) wa kufungiwa kufanya sanaa kwa muda usiojulikana, jambo ambalo siyo kweli.
MONDI ATOBOA SIRI Katika mahojiano na vyombo vya habari jijini Nairobi nchini Kenya hivi karibuni, Diamond ndiye aliyetoboa siri ya kuitwa kwake na JK kuwa alitaka kumpa wosia huo.
Diamond ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) alifunguka juu ya wosia huo kama ifuatavyo; “Nilipokuwa Mwanza (kwa ajili ya Tamasha la Wasafi), Rais mstaafu Jakaya Kikwete alinipigia simu na kunitaka niende nikamuone haraka.
“Kwenye mazungumzo yetu ya simu aliniuliza ninaendeleaje baada ya kuona video iliyokuwa inaonesha nikianguka jukwaani (kule Sumbawanga mkoani Rukwa) nilipokuwa ninapafomu.” Mondi au Simba alisema kuwa, baada ya kumalizana na JK kwenye simu, aliporejea jijini Dar akitokea Mwanza ndipo alipokwenda kumuona kiongozi huyo mstaafu anayependwa na wengi.
JAMBO LA KWANZA “Baadaye, nilikwenda nyumbani kwake (JK) jijini Dar. Pamoja na mambo mengine, nikiwa pale, kitu cha kwanza kabisa alinishauri nioe kwani umri unaruhusu (Diamond ana umri wa miaka 30 sasa). “Aliniambia ni muda muafaka kuoa na kutulia,” alisema Diamond na kuendelea:
JAMBO LA PILI “Pia alinionya juu ya kuposti video na picha kwenye mitandao ya kijamii zikionesha nikitandaza pesa mezani. “Hayo aliyasema baada ya mimi kuposti video kwenye Instagram ikimuonesha Tanasha (mpenzi mpya wa Diamond) na mimi tukiwa hotelini nikihesabu maburungutu ya pesa juu ya meza wakati Tanasha akipiga ‘selfie’ kwa kutumia simu janja.
“Rais huyo mstaafu aliniambia jambo hilo nililofanya halikuwa sahihi ukitegemea kwamba kuna watu hawana uwezo kabisa wa kimaisha ambao watajisikia vibaya kuniona mimi nikijionesha nina pesa.
JAMBO LA TATU “Aliniambia niwe makini na mambo ninayoyafanya kwani mengine yanaweza kunijengea chuki kwa watu.
“Aliniambia anaweza kuja mtu mbaya kunipongeza kwa mafanikio au jambo lolote, lakini siwezi kumjua kwani atakuwa anakuja mbele yangu akinichea usoni, lakini moyoni ana chuki.
“Kwa upande mwingine aliniambia ninaweza kupata matatizo ya kipesa, nitakapomfuata mtu mwenye chuki na mimi ataishia kunipa pole tu usoni, lakini ndani ya moyo wake atakuwa na furaha, hapo nitakuwa nimepata matatizo kwenye maisha yangu.”
GUMZO Kufuatia wosia huo kuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii, wengi wa waliousoma hasa mashabiki wa Diamond walimkomalia kuufuata kwani ndani yake una maonyo na mafundisho. “Suala la kujionesha kwenye video akihesabu pesa kweli halikuwa na picha nzuri hata kidogo.
“Kuna wengine hawana uwezo wa kupata hata mlo mmoja kwa siku, unapowaonesha pesa zako na kuzimwaga mezani, unawakwaza. “Ishu ya kuoa namuunga mkono JK kwani ni kweli kabisa umri wa Simba umekwenda hivyo aache kubadilisha wanawake kama nguo.
“Mimi namuunga mkono JK, Diamond awe makini sana na watu wanaomchekea, lakini moyoni wana chuki juu yake kwa sababu ya mafanikio yake,” ilisomeka sehemu ya maoni lukuki kwenye mitandao ya kijamii kuhusu wosia huo wa JK kwa Diamond.
KIFUATACHO… Juzi, Diamond aliendelea na shoo zake na kundi lake la WCB nchini Kenya ambapo baada ya hapo itafuata shoo kubwa jijini Dar ambayo inatarajiwa kutangazwa muda wowote kuanzia sasa.