NEWS

2 Januari 2019

Waziri Lukuvi: Misimamo ya Rais Magufuli Kuhusu Kulinda Rasilimali za Nchi Haijawafurahisha Wazungu

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya  Makazi, William Lukuvi, amesema chanzo cha baadhi ya nchi wahisani kugomea kutoa misaada kwa Tanzania kunatokana na msimamo wa Rais Dk. John Magufuli kuhusu kulinda rasilimali za nchi.

Kwa mujibu wa Lukuvi msimamo huo haujazifurahisha nchi hizo na kuamua kuweka masharti magumu katika misaada yao kwa Tanzania.

Waziri Lukuvi, alitoa kauli hiyo usiku wa kuamkia jana, wakati wa mkesha wa kukaribisha mwaka mpya  wa 2019, uliofanyika Kariakoo, Dar es Salaam ambapo alimwakilisha Rais Magufuli.

Waziri Lukuvi, alisema pamoja na hali hiyo, bado Serikali imeendelea kuwa imara na kuhakikisha inakusanya kodi za ndani ili kuweza kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwamo ya umeme wa maji wa Rufiji (Stiegler’s Gorge). 

“Leo (jana) tupo kwenye mkesha hapa, hakika nawaomba endeleeni kumwombea kwa dhati Rais Magufuli ili Mungu azidi kumpa nguvu na baraka za kuliongoza Taifa letu.

“Mnakumbuka hivi karibuni Tanzania kupitia Bunge, ilipitisha sheria ya kulinda rasilimali zetu za nchi (Sheria ya Madini ya mwaka 2017),baada ya kuanza kutumika mabwana wakubwa (wahisani) imewauma, sasa tunahitaji kujenga nchi inayokwenda kwa kasi kwa maendeleo na leo haya yote yanaonekana chini ya Rais Magufuli,” alisema Lukuvi.

Alisema pamoja na misimamo ya wahisani, bado Taifa linaendelea kupiga hatua kwa kasi ikiwamo kujenga miradi mkubwa kama wa reli ya kisasa (SGR).

Akizungumzia kero ya maji, alisema kwa sasa utekelezaji wa miradi ya maji kwa wananchi hali imekuwa ni nzuri huku lengo la Serikali ni kutaka kuona Watanzania wote wanapata huduma hiyo wakati wote.

Licha ya hali hiyo, alisema amekuwa akifanya mambo mengi makubwa  ambapo alitangaza kuanzia jana halmashauri zote zitaanza kutoa leseni za makazi kwa waliojenga kwenye maeneo ambayo hayajapangwa.

“Kuanzia kesho (jana) halmashauri zote ninaziagiza zianze kutoa leseni za makazi kwa wale waliojenga kwenye maeneo ambayo hajapimwa. Leseni hizo zitakuwa za miaka mitano na baada ya muda maeneo hayo yatapimwa na kupewa leseni. Lakini hata ukipewa leseni nenda kalipe kodi ya ardhi.

“Nami ninaawaambia Watanzania endeleeni kumwombea Rais Magufuli, maana hata sisi wasaidizi wake tumekuwa tukipata faraja kutokana na namna kiongozi wetu  anavyojitoa kwa ajili ya Watanzania.

“Tangu tumeingia madarakani, pale wizara ya ardhi hakuna migogoro mipya zaidi ile ya zamani ambayo ilikuwa inatengenezwa na watu wachache kwa masilahi yao.

“Tumuunge mkono Rais Magufuli tunataka nini, kila siku amekuwa akiweka mambo sawa sasa wafanyabiashara nchi nzima wamepewa vitambulisho aliyetenegeza ni Rais Magufuli twendeni tumuunge mkono kiongozi wetu kwa ajili ya Taifa letu,” alisema.

Akijibu hoja ya kuzuiwa kufanya maombi  Uwanja wa Taifa, Lukuvi alisema analichukua suala hilo na kulifikisha kwa Waziri wa Habari, Michezo, Sanaa na Utamaduni, Dk. Harrison Mwakyembe.

Awali akiendesha dua maalumu kwenye mkesha huo ,mwenyekiti wa mkesha mkubwa kitaifa, Askofu Dk. Godfrey Malassy wa Tanzania Fellowship of Churches, alishukuru serikali kwa upendo wake kwa Watanzania.

Pamoja na hali hiyo, waliwaombea viongozo mbalimbali, ikiwamo Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge, Job Ndugai pamoja na Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma.

Wengine waliombewa kwenye mkesha huo mawaziri, wabunge, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, wakuu wa mikoa na wilaya, viongozi wa dini pamoja na Watanzania wote.