NEWS

30 Aprili 2019

Bobi Wine arudishwa rumande Uganda

Kumekuwa na hisia kali kufuatia taarifa kwamba mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda, Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine amerudishwa rumande mpaka Mei 2 siku ya Alhamisi wiki hii.

Ameshtakiwa kwa kushiriki katika maandamano ya 'haramu' mnamo mwaka jana ya kupinga kodi ya kutumia mitandao ya kijamii maarufu Uganda kama OTT.

Alionekana akitembea huku akiwa amefungwa pingu mikononi kabla ya kuabiri basi la magereza kuelekea katika gereza kuu la Luzira mjini Kampala.



Ameshtakiwa kwa kuandaa maandamano ya umma kinyume na sheria, na alizuiwa siku ya Jumatatu katika kituo cha polisi cha Naggalama kwa mujibu wa taarifa ya polisi.

Msemaji wa idara hiyo Fred Enanga amesema Bobi Wine aliongoza maandamano hayo mwaka jana pasi kwanza kuomba ruhusa kutoka kwa polisi.

"Anazuiwa na polisi na uchunguzi unaendelea," ameliamba shirika la habari la AFP.

Kampeni mpya imeanzishwa katika mitandao ya kutaka Bobi Wine aachiliwe huru huku baadhi wakizungumzia hatua hiyo kama ya kutia wasiwasi.