LEO Jumapili hutakiwi kukosa pale Uwanja wa Taifa kwani mastaa Mbwana Samatta na Ally Saleh Kiba na timu zao watakuwa wakionyesha umwamba katika mchezo maalum uliopewa jina la Nifuate huku kila upande ukitamba kuwa lazima ushinde.
Mchezo huo ni maalumu, umeratibiwa na Samakiba Foundation kwa lengo la kuhakikisha wanarudisha shukrani zao kwa jamii yote hususani ile yenye mahitaji maalum na mechi ya kesho itakuwa ya pili kwani mwaka jana ilichezwa kwa mara ya kwanza.
Benchi la Timu Samatta litakuwa likiongozwa na Kocha Ammy Ninje ambaye ni Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF wakati Timu Kiba nayo imeleta Kocha kutoka Colombia aitwaye, Edwardo Tamiyo. Alikiba alisema;
“Nimemchukua kocha wa kigeni ili kuleta utofauti kidogo na kubwa zaidi ni kuongeza chachu na ladha ya mchezo huu ambao awamu hii mimi nitakuwa timu mwenyeji.
Wakati Kiba akimuweka wazi kocha wake, Samatta yeye alifanya siri, lakini Championi Jumamosi liliweza kupata taarifa kutoka kwa mwakilishi wa mmoja ya wadhamini wa mchezo huo ambaye hakutaka kutajwa ambapo alisema: “Timu Samatta itakuwa chini ya Ammy Ninje.”
CHEKI TAMBO ZAO SASA
Kwa upande wake Samatta alisema: “Najisikia faraja kubwa kuona Jumapili hii tunaingia tena kwa mara ya pili katika mchezo ambao mapato yake yatakwenda kusaidia jamii moja kwa moja ambapo msimu huu tumepanga kuyaelekeza kwa makundi ya watu maalumu.”
Kiba naye alisema: “Namshukuru Mungu kwa kutukutanisha kwa mara nyingine tena kuendeleza pale tulipoishia mwaka jana, kwani hii ina maana kubwa kwetu ya kudumisha ushirikiano ambao tuliamua kuungana na kufanya kitu kwa jamii ambazo zilikuwa zinahitaji kusaidiwa masuala mbalimbali.
“Mwaka huu tunaenda kupeleka zaidi mapato haya katika makundi ya watu tofauti na mwaka jana, ambapo tulipeleka misaada katika shule ya Mbagala Rangi Tatu aliyosoma mwenzangu Mbwana Samatta.
“Tumefanya hivi kama eneo la kusaidia au kuikumbuka jamii ambayo inakuwa na mahitaji muhimu, sisi ni watu ambao tunakubalika na jamii hivyo tukaona siyo jambo baya kurudisha kitu kidogo kwa jamii yetu.”
Samatta Atembelea Global Group, Aomba Mashabiki Wafurike Taifa
The post Samatta, Kiba Hapatoshi Leo Taifa appeared first on Global Publishers.