NEWS

31 Julai 2019

Waziri wa Kilimo Mhe Hasunga Aitaka NFRA Kutoa Elimu Ya Mifuko Ya Pic's Kwa Wakulima

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Simiyu
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga jana tarehe 30 Julai 2019 ametembelea na kujionea maandalizi ya Maadhimisho ya 27 ya sikukuu ya wakulima maarufu kama (Nane Nane) yenye lengo la kuwatambua na kuwaenzi Wadau Wakuu wa Sekta ya Kilimo ambao ni Wakulima, Wafugaji, Wavuvi, Wanaushirika, Wasindikaji wa mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na maliasili kwa mchango wao mkubwa wanaoutoa katika kuendeleza uchumi wa nchi yetu.

Mhe Hasunga pamoja na mambo mengine akiwa katika Banda la Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ameutaka uongozi wa taasisi  huyo kuongeza juhudi za utoaji elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya mifuko maalumu ya kuhifadhia nafaka ya PIC'S.

Mhe Hasunga amesema kuwa NFRA inapaswa kutoa elimu hiyo ili iwafikie wakulima wengi kwani kufanya hivyo itarahisisha huduma za uhifadhi wa mahindi ya wakulima ambao kwa muda mrefu wamekumbwa na kadhia ya kushindwa kuhifadhi mahindi kwa ufasaha.

Pamoja na NFRA kutoa elimu kwa wakulima kupitia vipindi mbalimbali vinavyorushwa na Televisheni lakini pia amesisitiza kuwa NFRA inapaswa kuongeza uwezekano wa kuwafikia wakulima wengi zaidi.

Mwaka huu wa 2019, sherehe za Nanenane zinafanyika Kitaifa mjini Bariadi katika Viwanja vya maonesho ya kilimo Nyakabindi katika Mkoa wa Simiyu hivyo Mhe Hasunga amepongeza Uongozi wa mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara kwa juhudi zao za kufanikisha kuingiza uwanjani huduma za msingi ambazo ni maji na umeme.

Alisema kuwa jukumu hilo kwa Serikali na Wadau wa Sekta Binafsi ni kuendeleza viwanja hivyo vya Nyakabindi kwa kujenga mabanda ya maonesho ya kudumu na kuboresha huduma muhimu za kijamii ili kuwe na maonesho endelevu yenye sura ya Kitaifa na Kimataifa.

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA pamoja na Taasisi zingine za wizara ya Kilimo zimetuama Mkoani Simiyu kwa ajili ya kutoa elimu kwa wakulima kuhusu majukumu wayafanyayo kadhalika namna bora ya kuwa na Kilimo bora na chenye tija.

MWISHO.