NA SALVATORY NTANDU
Mtu mmoja ambaye hajafahamikia jina wala makazi mwenye umri kati ya miaka (35-40) amefariki dunia na mwingine kujeruhiwa baada ya pikipiki aliyokuwa amepanda kugongwa na gari aina ya SUZUKI VITALA lenye namba za usajili T 432 ALT likiendeshwa na Salum Saidi (30) mkazi wa Mwanza.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga (ACP) Richard Abwao amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa ajali hiyo imetokea jana katika eneo la Ushirika, barabara ya Shinyanga kuelekea Mwanza, Manispaa na Mkoa wa Shinyanga.
Amesema dereva wa gari hilo Salum ameumia kifua, aliigonga pikipiki yenye namba za usajili T 295 BSG aina ya kiboko iliyokuwa ikiendeshwa na Kishimba Sanzago (28) mkazi wa Ibadakuli ambaye ameumia kichwani huku abiria wake akifariki dunia ambaye bado hajafahamika jina wala makazi.
Kamanda Abwao amesema Majeruhi anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga na mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitalini hapo na chanzo cha ajali hiyo ni ulevi kwa dereva wa gari hilo na amekamatwa huku vyombo husika vipo kituoni.