NEWS

1 Agosti 2019

EU Watoa Neno Kifo cha Mtumishi Wizara ya Fedha



Umoja wa Ulaya (EU) umesema umeshtushwa na kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Fedha za Nje wa Wizara ya Fedha na Mipango, Mhandisi Leopold Lwajabe, ambaye mwili wake ulikutwa ukining'inia juu ya mwembe katika kijiji cha Mgoza Wilayani Mkuranga siku ya Julai 26, 2019.


''Tumesikitishwa na taarifa za kifo cha Lwajabe, ni mwenzetu, ni rafiki yetu mzuri, kifo chake kimetustua sana'', imesema taarifa ya EU.

Aidha taarifa hiyo imebainisha kuwa utendaji na kujitoa kwake katika kazi kwa miaka kadhaa ni wa kuthaminiwa na wako bega kwa bega katika kutoa ushirikiano wao kwa ndugu na Wizara ya Fedha katika kipindi hiki kigumu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya DSM leo Julai 31, imeeleza kuwa Lwajabe alijinyonga huku akiacha ujumbe wa wosia ofisini juu ya meza yake akitoa mgawanyo wa mali kwa ndugu zake ikiwemo mashamba, nyumba, gari, ng'ombe na viwanja.

Wosia mwingine aliouacha ni wa kuchinjiwa ng'ombe takribani wanne wakati wa maombolezo ya msiba wake.