NEWS

3 Agosti 2019

Jeshi la Polisi Latoa Mafunzo Kwa Wahudumu Wa Mkutano Wa SADC

Tunapoelekea katika Mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC na kuhakikisha mkutano huo unakua wa mafanikio na kuiletea sifa nchi yetu, Jeshi la Polisi Tanzania limepewa fursa ya kutoa mafunzo ya utayari kwa wahudumu watakaoshiriki kutoa huduma za msingi kwa wajumbe wakati mkutano huo ukiendelea ambao unaotarajiwa kuanza tarehe 17 na 18 mwezi huu.

Mkuu wa Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi DCP Ali Lugendo amesema mafunzo hayo yanayohusisha wanafunzi 71, yatawasaidia kuwajengea uwezo wa kiuzalendo na nidhamu na kuwa mabalozi wazuri kwa wageni watakaohudhuria katika mkutano huo katika masuala ya utalii.

Naye Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam, Naibu Kamishna wa Polisi DCP Anthony Rutashuburugukwa alisema kuwa ni heshma kwa Jeshi la Polisi kupata fursa ya kutoa mafunzo kwa wahudumu wa wageni wa kimataifa.

Katika mafunzo hayo yanayofanyika katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam yanahusisha wanafunzi 71 kutoka vyuo mbali mbali hapa nchini vikiwemo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo cha Diplomasia, Chuo Kikuu cha Zanzibar, Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), Chuo cha Uhasibu Arusha pamoja na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).