NEWS

30 Desemba 2019

Serikali Yavunja Mkataba Na Kurejesha Umiliki Wa Machinjio Ya Dodoma

Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Luhaga Mpina, amesema Serikali imevunja mkataba wa mauzo ya mali za machinjio ya Dodoma baina ya Serikali na Kampuni ya Uwekezaji wa Taifa (NICOL) uliosainiwa mwaka 2008 kutokana na kampuni hiyo kusababisha hasara ya shilingi bilioni 9.7

Sambamba na hilo, vyombo vya ulinzi na usalama vimeagizwa kuwachukulia hatua za kisheria watendaji wote wa NICOL, NARCO na TMCL waliohusika na ubadhirifu wa mali za TMCL na kuisababishia hasara serikali tangu mwaka 2008.

Hatua hiyo ilifikiwa jana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, katika kikao cha wadau kujadili namna ya kunusuru machinjio hayo.

Mpina alisema mkataba huo umevunjwa kwa kuzingatia ibara ya 7 na 13 ya mkataba wa mauzo ya mali na hivyo kuanzia sasa machinjio hiyo itakuwa chini ya serikali.

“NICOL ilipe serikali Sh. 9,712,127,660 ambazo serikali ilipunjwa katika biashara ya machinjio na pia NICOL ilipe madeni yote inayodaiwa kampuni ya ubia TMCL kiasi cha Sh. 5,248,084,000,” alisema.

Aidha, aliitaka kampuni ya NARCO ijiondoe katika kampuni ya Ubia TMCL ndani ya siku 60 kuanzia jana.

“Huduma za uchinjaji zitaendelea kutolewa kama kawaida katika kipindi cha mpito chini ya usimamizi wa serikali wakati mchakato wa kumpata mwekezaji mahiri wa mpito na wa kudumu unaendelea,” alieleza.