Mwanza. Tukio la kukamatwa, kuhojiwa na kushikiliwa kwa muda na kabla ya kuachiwa kwa wasaidizi wa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika umeibua mgongano kati ya Jeshi la Polisi Tanzania na chama hicho.
Mgongano huo umeibuka baada ya pande hizo mbili kutaja eneo tofauti la tukio na sababu za kukamatwa kwa watu hao ambao ni Ofisa Habari wa Chadema na Msaidizi binafsi wa Mnyika, Abdulkarim Muro na dereva wa Katibu Mkuu huyo, Said Haidan.
Wakati Jeshi la Polisi kupitia kwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro inadai maofisa hao wa Chadema walikamatwa kwenye nyumba moja jirani na Hoteli ya Paradise eneo la Mahina jijini Mwanza, Chadema wao wanadai ukamataji ulifanyika ndani ya hoteli hiyo.
Pande hizo pia zimetofautiana sababu za ukamataji kwa Polisi kudai ulitokana na taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu kuwepo wa watu wanaohisiwa kuwa ni wahalifu wakati Chadema wanadai maofisa wake walikamatwa kama sehemu ya kumsaka Katibu Mkuu wake, John Mnyika aliyekuwa jijini Mwanza kwa mapumziko na shughuli za kifamilia.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari leo Desemba 30, 2019, Kamanda Muliro amesema maofisa hao waliokamatwa Desemba 29, 2019 walikutwa kwenye nyumba moja iliyo karibu na hoteli ya Paradise eneo la Mahina jijini Mwanza kutokana na taarifa kutoka kwa raia wema.
“Baada ya taarifa hizo, jeshi la polisi lilifanya ufuatiliaji wa haraka na kuwakamata watu hao wawili ambao katika mahojiano ya awali walikataa kutoa utambulisho wao kuwa ni akina nani na wamefika maeneo hayo kufanya shughuli gani,” inasema taarifa hiyo
“Hivyo jeshi la polisi liliwachukua na kuwapeleka kituo cha kati ambapo hata hivyo baadaye walitoa ushirikiano kwa askari na kutaja majina yao,” inaeleza zaidi taarifa hiyo
Anasema baada ya kujiridhisha kuwa watu hao hawakuwa wahalifu, Polisi iliwaachia huru.
Maelezo ya Chadema
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Desemba 30, 2019, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema taarifa ya polisi imepotosha kuhusu eneo la tukio na sababu za kukamatwa kwa maofisa wa chama hicho.
“Maofisa wetu ambao wako Mwanza na Katibu mkuu (John Mnyika) kwa mapumziko na shughuli ya kifamilia walikamatwa wakiwa ndani ya eneo la hoteli ya Paradise; taarifa ya polisi kuwa waliwakamata nyumba jirani na hoteli inaibua hisia ya nia ovu katika tukio hili,” amesema Mrema na kuongeza
“Hata madai kuwa walihisiwa kuwa wahalifu siyo sahihi kwa sababu baada ya kuwakamata (polisi) waliwahoji kuhusu alipokuwa katibu Mkuu, John Mnyika,”
Pamoja na kulaani kitendo hicho, Mrema ameiomba jeshi la Polisi kufanya kazi kwa weledi bila kujiingiza kwenye masuala ya kisiasa kwa kuwadhibiti viongozi, wanachama na wafuasi wa vyama vya upinzani.
“Mbona Katibu Mkuu wa CCM (Chama Cha Mapinduzi) anazunguka kila sehemu nchini akifanya vikao vya ndani na kuhutubia mikutano ya hadhara bila kubughudhiwa na polisi ambao huonekana wakisindikiza msafara wake,” amehoji Mrema.
Mwananchi