NEWS

30 Januari 2020

Polisi mkoani Shinyanga yamshikilia mtu mmoja kwa kujifanya ofisa usalama wa Taifa

Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linamshikilia mkazi wa Shinyanga mjini, Sheliku Sweya (45), kwa tuhuma ya kujifanya ofisa usalama wa Taifa, kutapeli fedha watumishi wa umma, kuomba rushwa ya ngono.

Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Deborah Magiligimba, alisema mtuhumiwa huyo kwa nyakati tofauti amekuwa akitembelea ofisi za umma na kuanza kutapeli watumishi na kwamba alifanikiwa kumtapeli Mganga wa Hospitali ya Rufani mkoani Shinyanga, Geofrey Mboye, kiasi cha Sh. 300,000.

Kamanda Magiligimba alisema mtuhumiwa huyo alifika kwenye hospitali hiyo na kuonana na mganga huyo na kujitambulisha kuwa ni ofisa usalama wa Taifa na atamsaidia shida zake.

“Ndipo akamwambia amsaidie kumhamisha kutoka Shinyanga kwenda Dodoma na kuombwa kiasi hicho cha fedha na kutapeliwa,” alisema Kamanda Magiligimba.

Alisema mtuhumiwa huyo hakuishia hapo pia alikwenda kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Rose Malisa, ambaye alimuomba rushwa ya ngono kwa ahadi ya kumtatulia changamoto zilizopo hospitalini hapo, ikiwamo kupatiwa vifaa tiba pamoja na kuongezewa watumishi wa afya.

“Mtuhumiwa alimuahidi mganga huyo kuwa atamfutia deni analodaiwa na taasisi ya afya alikopata masomo ya udaktari wa magonjwa bingwa ya kinamama kiasi cha Sh. milioni 40 ndipo akamshitukia na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi na kuwekewa mtego na kufanikiwa kukamatwa,” alisema Magiligimba.

Alisema baada ya mganga huyo kuwa na shaka, alitoa taarifa Jeshi la Polisi ambalo liliweka mtego wa rushwa hiyo ya ngono, na kabla ya mtuhumiwa kufanikiwa kupata rushwa hiyo alikamatwa.

Alisema walipofanya uchunguzi walibaini kuwa siyo ofisa usalama wa Taifa.

Kamanda Magiligimba alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchuguzi juu ya mtuhumiwa huyo, upelelezi ukikamilika, atafikishwa mahakamani.