NEWS

30 Januari 2020

Waziri Mkuu Atoa Ufafanuzi Changamoto za NIDA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali imeongeza watumishi wa NIDA pamoja na vifaa ili kuondoa changamoto kwa Watanzania za kupata vitambulisho vya uraia.

Amesema hayo leo Alhamisi  akiwa katika kipindi cha Maswali na majibu kwa Waziri Mkuu Bungeni.

“Watanzania wengi tulikuwa hatujawafikia kuwapa vitambulisho vya NIDA mpaka ngazi ya vijiji na kule vitongojini, jambo hili Serikali imelifanyia kazi kwanza tumeongeza idadi ya watumishi kwenye ngazi ya Halmashauri, pili tumeongeza mitambo ya kufanyia kazi.
 
“Yako maeneo tumeongeza umakini mkubwa hasa maeneo ya mipakani kwa lengo la kuzuia wananchi wa Nchi jirani kujipatia kitambulisho cha NIDA nchini Tanzania halafu akafanya mambo yake huku ndani kupitia kitambulisho cha nchi kwa hiyo mtaona kunaweza kuwa na uchelewashwaji huko kwenye miji iliyoko mipakani na nchi jirani na Tanzania kwa sababu tunafanya zoezi ili kwa umakini kwa lengo la kutoa kitambulisho kwa mtanzania tu” - Amesema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa