NEWS

31 Januari 2020

Waziri Mkuu Atoa Ufafanuzi Changamoto za NIDA


Mbunge wa Buhigwe, Obama Ntabaliba (CCM), ameibua suala la ugumu wa upatikanaji wa vitambulisho vya taifa vinavyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) bungeni ambapo ametaka kauli ya serikali katika kuharakisha upatikanaji wa vitambulisho hivyo.

Mbunge huyo alikuwa akiuliza swali katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

“Natambua juhudi za serikali juu ya upatikanaji wa vitambulisho vya taifa, vile vile natambua na najua umuhimu wa vitambulisho hivyo kwa Watanzania na sababu za kiusalama, lakini vile vile kwa sasa hivi kumekuwa na changamoto katika upatikanaji wa namba za NIDA kwenye vijiji na miji, nini kauli ya serikali kwa sababu wananchi sasa wanapata mkanganyiko uharaka na upatikanaji, nini kauli ya serikali,” amehoji.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu swali hilo amesema ukweli wa suala hilo ni kwamba Watanzania wengi walikuwa hawajafikiwa kupata vitambulisho kutoka ngazi ya vijiji na vitongojini lakini jambo hili serikali imelifanyia kazi.

“Kwanza tumeongeza watumishi kwenye ngazi ya halmashauri ili kurahisisha kazi hiyo, lakini pili tumeongeza watumishi kwenye ngazi za halmashauri ili kuwezesha kufikika kwenye halmashauri hadi vitongoji na kufanya kazi hiyo lakini pia tumeongeza pia na mitambo ya kufanyia kazi ili baadaye tuweze kupata vitambulisho na idadi hii ya watumishi ambao tumewaongeza ni hadi makao makuu ili kuweza kuharakisha vile vitambulisho.

“Kama Mtanzania anahitaji huduma yoyote ile inayohitaji kitambulisho cha Nida, serikali imeridhia kama mwananchi atakuwa hajapata kitambuliso cha Nida basi atumie namba aliyopewa ili kuweza kuhalalisha kupata huduma yoyote ile ambayo inahitaji kitambulisho huku akiwa hana kitambulisho hiyo ni njia ya kwanza ambayo tumetumia kurahisisha kuwafikia Watanzania.

“Lakini inawezekana namba hii ni ngumu kwa mwananchi huyu aliyeko kijijini kuipata, tumetoa maelekezo kwa watumishi wetu wa Nida walioko kule ngazi ya halamsahuri kwamba watoe orodha kwa wale wote waliowaandikisha katika vituo vyao na namba zao ili angalau mwananchi aweze kuifikia kwa hiyo afike pale kwenye kituo aone namba yake sasa imuwezeshe kupata huduma popote panapohitaji kitambulisho cha Nida kwa kupeleka namba tu, hiyo ndiyo njia tumerahishsiha kuwafikia Watanzania wote hadi kijijini kwa haraka,” amesema.

Aidha, Majaliwa amesema yako maeneo serikali imeongeza umakini mkubwa hasa maeneo ya mipakani kwa lengo la kuzuia wananchi wa nchi jirani kujipatia kitambulisho cha Nida kuja nchini kisha akafanya mambo yake huku ndani kupitia kitambulisho cha nchini.

“Kwa hiyo mtaona kunaweza kuwa kuna ucheleweshaji upo kwenye miji iliyopo mipakani na nchi jirani za mipakani kwa sababu tunafanya zoezi hili kwa umakini tunatoa kitambulisho kwa Mtanzania tu na nitoe wito kwa Watanzania mtusaidie kuwaambia ambao si wakazi wa nchi wanaokuja nchini kuchukua vitambulisho vyetu kwa lengo la kudhibiti hali ya ulinzi na usalama ndani ya nchi.

“Kwa hiyo kama kunaweza kuwa na ucheleweshaji kwenye baadhi ya maeneo kadhaa hasa mipakani hasa Buhigwe ambako mheshimiwa Obama anatoka ni karibu na Burundi ni ili tusiweze kutoa vitambulisho kwa wageni,” amesema Majaliwa.