NEWS

30 Aprili 2020

Afariki Dunia kwa Kukanyagwa na Tembo



RAJABU WEJE (43) mkazi wa Kijiji cha Angalia kata ya Mtina Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma amefariki Dunia kwa kukanyagwa na Tembo shambani kwake wakati akilinda mazao ya shambani humo yasiharibiwe na wanyama hao.

Akizungumza ofisini kwake kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Simon Maigwa amelitaja tukio hilo kuwa limetokea Aprili 27 mwaka huu majira ya saa moja na nusu wakati marehemu akiwa shambani hapo.

Kamanda Maigwa amesema kuwa Marehemu Rajabu Weje alipatwa na mkasa huo alipokuwa akilinda mazao yake yaliyopo shambani ili yasiliwe na wanyama gafla alitokea mnyama Tembo kwenye shamba hilo na kuanza kumshambulia kwa kumkanyaga sehemu mbalimbali za mwili hadi kumsababishia kifo papo hapo.

Maigwa amesema kuwa marehemu huyo katika shamba lake alikuwa akilima mazao mchanganyiko ambayo ni Mahindi,Mpunga,Karanga na Viazi na kuwa muda wa mavuno alikuwa akiishi hukohuko kwenye kibanda alichokuwa amekijenga shambani humo.

Amefafanua kuwa mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na madaktari wa Hospital ya Wilaya ya Tunduru na kukabidhiwa kwa ndugugu zake tayari kwa mazishi .