NEWS

10 Septemba 2020

Afrika Kusini yamkemea Trump kwa kauli yake ya kumdharau Mandela



Chama tawala cha Afrika Kusini -South African National Congress (ANC) kimemuita rais wa Marekani Donald Trump kuwa mtu “anayesababisha uhasama, mwenye chuki dhidi ya wanawake na asiye na heshima ” kilipokuwa kikijibu ripoti kwamba alimpuuzilia mbali Nelson Mandela , rais wa kwanza mweusi wa taifa hilo.

Bwana Trump alisema kuwa mshindi wa tuzo ya amani “hakuwa kiongozi “, kwa mujibu wa wakili wake wa zamani Michael Cohen.


Madai hayo yanatoka katika kitabu kipya cha Cohen -Disloyal: Kitabu kinachoelezea maisha yake. Ikulu ya Marekani White House inasema kuwa Cohen ni muongo.


Kitabu chake pia kinasema kwamba Bwana Trump ana tabia kama za mjumbe wa kikundi kinachofanya ghasia za uhalifu na “anawadharau watu wote weusi “

Katika jibu lililojaa ukosoaji, chama cha ANC, ambacho Mandela alikiongoza kuanzia mwaka 1991 hadi 1997, kilisema kwamba “watu wote wanaopenda uhuru wa dunia wanasikitishwa sana na matusi haya ambayo yanatoka kwa mtu ambaye binafsi hana uwezo wa kuwa kiongozi wa mfano wa kuigwa “.

“Trump ni mtu anayesababisha uhasama, anayewachukia wanawake na asiye na heshima kuwahi kuchukua wadhifa wa rais,” iliongeza.

Kinyume chake, Mandela alisimama kama kiongozi aliyewaunganisha watu, ambaye “alifika katika maeneo mbali mbali ya dunia na kuleta amani na haki ya jamii “, ANC ilisema.


Mshindi wa Nobel ya amani

Mandela, ambaye alifungwa jela kwa miaka 27 kwa mapambano yake dhidi ya ubaguzi wa rangi, alifanya mazungumzo na serikali ya wazungu walio wachache kuhakikisha kunakuwa na kipindi cha mpito cha bila ghasia kuelekea utawala wa kidemokrasia mwaka 1994.


 


Mwaka 1993, alishinda tuzo ya amani ya nobel pamoja na rais wa zamani wa Afrika Kusini FW de Klerk, mtu ambaye alifanya nae mazungumzo, kwa juhudi zao za kumaliza “utawala wa ubaguzi wa rangi kwa amani “.


Ubaguzi wa rangi ulikua ni mfumo uliokubalika kisheria dhidi ya watu ambao hawakuwa wazungu, na ulianzishwa nchini Afrika Kusini mwaka 1948.


Michael Cohen alifanya kazi kama wakili wa kibinafsi wa rais Donald Trump

Mandela alikuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini na akaondoka madarakani mwaka 1999. Alifariki dunia mwaka 2013 akiwa na umri wa miaka 95.


Awali, Wakfu wa Nelson Mandela ulisema kuwa hauamini kwamba “viongozi wenye haiba kama aliyonayo Trump wako katika nafasi ya kutoa kauli za kimamlaka juu ya maisha na kazi ya Madiba [Mandela]”.


Pamoja na kumkosoa Mandela, rais wa Marekani aliripotiwa na Cohen kuwa alisema : “Niambie nchi hata moja inayoendeshwa na mtu mweusi ambayo sio shimo la uchafu . Zote ni uchafu kabisa .”


 


Kwa mujibu wa BBC. Maneno hayo yanafanana na madai sawa yaliyotolewa mwaka 2018, ambapo Trump aliyaelezea mataifa ya Afrika kama mataifa ya ”mashimo machafu”


Wakati huo, Bwana Trump aliwaambia waandishi wa habari: “Mimi sio mbaguzi. Mimi ni mtu mwenye ubaguzi wa kiwango cha chini mliyewahi kumuhoji.”


Akijibu kuhusu kitabu cha Cohen, afisa habari wa Ikulu ya White House, Kayleigh McEnany mwishoni mwa juma alimuelezea kama “mtu asiye na thamani, wakili aliyefukuzwa kazi, aliyelidanganya bunge la congress “.

“Amepoteza uaminifu wote, na si jambo la kushangaza kuona jaribio lake la hivi karibuni la kufaidika kutokana na uongo,” alisema