NEWS

10 Septemba 2020

Kikwete: Wapinzani Wameishiwa Hoja, Chagueni CCM Iendelee Kuwaletea Maendeleo

Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, amekoleza moto kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku akisema Watanzania wanapaswa kuendelea kukiamini chama hicho ili kushika dola.

Amesema CCM inastahili kupewa tena nafasi ya kuongoza ili kuwatumikia wananchi na kudumisha amani, upendo na kuwaletea maendeleo wanayoyahitaji.

Sambamba na hayo, Kikwete aliwaomba wananchi kutokubali kuyumbishwa na maneno ya wapinzani kwa kile alichodai wameishiwa hoja kwa kuwa yote wanayosema ni yale yaliyopita, ambayo CCM imeshayafanya muda mrefu.

Kikwete alitoa ahadi hiyo juzi wakati wa uzinduzi wa kampeni kwa nafasi za ubunge na udiwani mkoa wa Lindi, zilizofanyika katika uwanja wa Ilulu mjini hapa.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano, mgombea urais wa CCM, Rais John Magufuli amefanya mambo mengi mazuri ya kimaendeleo, ikiwamo uboreshaji huduma za afya, elimu, nishati na utoaji mikopo kwa vijana na kinamama.

Katika kipindi hicho, alisema kwa mkoa wa Lindi pekee zimejengwa hospitali mbili za wilaya, vituo vya afya 16 na zahanati 70 zimeboreshwa katika halmashauri zote sita.

Licha ya uboreshaji wa huduma hizo, pia alisema mikopo 4,693 yenye thamani ya Sh. 2,313,534,500 imetolewa kwa vijana, kinamama, na watu wenye uhitaji maalum kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) na halmashauri za wilaya na manispaa.