NEWS

12 Septemba 2020

Lissu Amuweka Njia Panda Bernard Membe


Mbio kuelekea Uchaguzi Mkuu, unaotarajiwa kufanyika oktoba 28, mwaka huu, zinazidi kushika kasi, huku mgombea urais kupitia Chama cha Chadema, Tundu Lissu, akizidi kumuweka katika wakati mgumu mgombea urais kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Bernard Membe kuhusu ushirikiano baina ya vyama hivyo viwili.



Hatua hiyo imekuja baada ya ushirikiano baina ya vyama hivyo, kuendelea kuwa kitendawili, licha ya viongozi wa vyama hivyo kila mara kujinasibu kuungana, huku wakiendelea na michakato mbalimbali ya uchaguzi.



Licha ya Membe kusisitiza ACT-Wazalendo kuwa itaungana na Chadema, tayari amechukua na kurejesha fomu za kuwania nafasi hiyo ya urais na kuendelea na kampeni kama anavyofanya Lissu, ambaye anawakilisha Chadema.



…AMTEGA MEMBE

Hata hivyo, katika kile kinachoonekana kumtega Membe, Lissu, alitangaza kuwa Chadema inamuunga mkono Mgombea urais wa ACT-Wazalendo, Maalim Sief Sharif Hamad katika kinyang’anyiro cha urais visiwani Zanzibar.



Akihutubia mkutano wa kampeni mjini Unguja mapema wiki hii, Lissu alisema Maalim Seif ndiyo mgombea pekee ambaye anaweza kuishinda CCM Zanzibar.“Mtu pekee na chama pekee chenye uwezo wa kuishinda CCM Zanzibar, kiongozi wa Wazanzibari, ni Maalim Seif.



Huyo ndiye mtu ambaye sisi Chadema tutamuunga mkono.“Hajawahi kubadilisha msimamo. Alianza akiwa kijana, leo ni mzee lakini msimamo wake juu ya Zanzibar, haujatetereka. Huyo ndiyo mtu ambaye anayeweza kuishinda CCM Zanzibar na huyo ndiyo mtu ambaye sisi Chadema tutamuunga mkono,” alisema Lissu.



Ingawa hakusema moja kwa moja kwamba Chadema inamuondoa mgombea wake Zanzibar, Said Issa Mohammed katika kinyang’anyiro hicho, matamshi ya Lissu yana maanisha kuwa, Chadema haitamnadi mgombea huyo na badala yake, itaungana na ACT-Wazalendo kumnadi Maalim Seif katika kuwania urais wa Zanzibar.



Mgombea urais wa chama tawala cha CCM Zanzibar ni Dk Hussein Mwinyi, ambaye alikuwa Waziri wa Ulinzi katika awamu ya kwanza ya Rais John Magufuli katika Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.



Kutokana na hali hiyo, wachambuzi wa siasa wameitafsiri hatua hiyo kuwa mtego kwa Membe, kwamba naye akubali kumuachia Lissu upande wa Bara. Mtihani huo mzito kwa Membe unajiri, ilhali viongozi wa pande zote mbili wakisisitiza mazungumzo kuwa yanaendelea baina yao.Kampeni za uchaguzi wa urais na wabunge Zanzibar, zinaanza rasmi Septemba 11.



MAJINA YAO NEC KIZUNGUMKUTI

Aidha, mtego mwingine ambao unadaiwa kumuweka Membe kwenye wakati mgumu, ni majina yake yaliyopo kwenye mfumo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ambao sasa utaweka majina yake katika orodha ya wagombea urais katika uchaguzi huo, hata kama ikitokea akajitoa kugombea.Mmoja wa wachambuzi wa siasa nchini, Aman Mbarouk alisema iwapo ikitokea Membe akajitoa kwenye uchaguzi huo, ina maana kuwa itahitaji nguvu kubwa kwenye mikakati ya kampeni, kuwaelimisha wananchi kuwa mgombea urais wa vyama hivyo viwili ni Lissu.



“Kwa sababu tayari mfano mzuri ulionekana katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ambapo wagombea ubunge na udiwani, walivurugana baada ya majina yao kuwepo kwenye fomu za uchaguzi, licha ya vyama vyao kumteua mgombea mmoja,” alisema.Mbarouk alisema kwa utaratibu ulivyo, NEC haitoweza kutoa tena majina yao kwenye uchaguzi huo, hasa ikizingatiwa iwapo wakiungana kwa ridhaa, muungano wao hautotambulika kwa mujibu wa sheria za uchaguzi.



MDORORO WA KAMPENI

Aidha, mdororo wa kampeni katika uchaguzi mkuu mwaka huu, pia unatajwa kuwa mojawapo ya mtego kwa Membe.Mdororo huo kwanza umesababishwa na gharama za uchaguzi ambazo vyama vyote vya siasa hujigharamia kwa njia mbalimbali. Hata hivyo, katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, nchi ambazo hutoa fedha za misaada kwa vyama kushiriki kwenye uchaguzi, zinadaiwa kuweka kusitisha michango yao kwa kile kinachoelezwa kuwa ni mdororo uliotokana na janga la maambukizi ya Virusi vya Corona.



Tayari, Membe ameonja shubiri ya mdororo huo katika kampeni zake kwa kukosa hamasa ya washiriki wengi katika mikutano yake kutokana na uwepo hafifu wa matangazo ya kutosha kuhusu mikutano yake.Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wachambuzi wamebainisha kuwa sasa ni muda sahihi kwa Membe kumuachia Lissu ambao licha ya kuweka wazi kuwa anahitaji fedha za kampeni, bado uwingi wa watu katika mikutano yake unazidi kuongezeka kutokana na hamasa aliyonayo kwa Watanzania.



ACT WAZALENDO: NI DALILI NZURI

Wakati hayo yakijiri, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Addo Shaibu alisema licha ya kwamba maamuzi aliyoyatangaza Lissu kuwa Chadema wanamuunga mkono Maalim Seif Zanzibar, si maamuzi rasimu, bado ni dalili nzuri kuelekea mazungumzo ya pande zote mbili.“Hadi sasa hakuna chama ambacho kimewatoa wagombea wake wa urais, ubunge au udiwani. Ninachoona ni dalili nzuri kuelekea ushirikiano wa vyama vyetu,” alisema Shaibu.

Stori: MwandiShi wetu,iJuMaa