Ujenzi wa Hospitali ya Uhuru Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma imekamilika kwa asilimia 87 baada ya Serikali kutekeleza ahadi yake ya kuzielekeza takribani Sh. bilioni 2.3 zilizotolewa na Kampuni ya Bharti Airtel ya India kujenga Hospitali hiyo.
Hayo yalibainishwa na Mhandisi wa Ujenzi wa jengo la Hospitali ya Uhuru, Bw. Girimu Kanansi, wakati Afisa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Bw. Jackson Mmbando, alipotembelea hospitali hiyo kuangalia maendeleo ya ujenzi wake, Mkoani Dodoma
Bw. Kanansi alisema kuwa jengo hilo lililokamilika kwa asilimia 87 linajengwa kwa weledi mkubwa na Kampuni ya Suma JKT kupitia vijana wazalendo wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kinyume na awali ambapo majengo makubwa kama hayo yalikuwa yanajengwa na kusimamiwa na wageni kutoka nje ya nchi.
“Kazi inayoendelea ni kutengeneza sakafu, kuweka mifumo ya umeme na kuskimu kuta, hivyo ninaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano na Kampuni ya Mawasiliano ya Airtel kuona umuhimu wa kupeleka huduma za Afya karibu na wananchi hususani mkoani Dodoma ambako ndio makao Makuu ya nchi”, alieleza Mhandisi Kanansi.
Alisema kuwa Jengo hilo lilitarajiwa kukamilika mwezi mei mwaka huu, lakini ilishindikana kutokana na changamoto ya msimu wa mvua kali ambao ulisababisha kutokuwa na mazingira Rafiki ya kusafirisha vifaa kwenda eneo la ujenzi.
Aidha kutokana na hali hiyo Mkandarasi aliomba kuongezewa muda, ambapo anatarajia kukamilisha ujenzi Oktoba mwaka huu iwapo hakutakuwa na changamoto yeyote itakayojitokeza ikiwemo ya kutofika kwa vifaa vya ujenzi kwa wakati.
Kwa upande wake Afisa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Bw. Jackson Mbando, alisema kuwa Kampuni yake imekuwa na utaratibu wa kutembelea eneo hilo la ujenzi ili kuona maendeleo yake kwa kuwa ni sehemu ya kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo hususani miradi ya Afya ikiwemo Hospitali ya Uhuru ambayo kupitia Mbia mwenza Bharti Airtel ya Tanzania ndio iliyotoa kiasi cha Sh. bilioni 2.3 kwa Serikali ambayo ilizielekeza katika ujenzi wa hospitali.
Alisema Kampuni ya Airtel Tanzania kwa kutambua uhitaji wa huduma ya Mawasiliano, tayari imefungua maduka manne Wilayani Chamwino likiwemo eneo la Hospitali ya Uhuru ambayo yataendelea kutoa huduma ikizingatiwa kuwa baadaya ya hospitali kuanza kufanya kazi huduma za fedha zitahitajika.
Akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa Kampuni ya Airtel Tanzania ikitoa Gawio kwa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James alisema kuwa, Serikali ya Tanzania ilianza uchunguzi wa umiriki wa Airtel Tanzania na baadae kufanya mazungumzo na Kampuni mama ya Bharti Airtel ya India kuanzia mwaka 2018 na kufanikisha Serikali kumiliki asilimia 49 ya hisa za kampuni hiyo.
Alisema makubaliano hayo yaliyosababisha kunufaika kwa pande hizo mbili ndiyo yalimfanya Mwenyekiti wa Bharti Airtel ya India, Bw. Sunil Mittal kutoa Sh. bilioni 2.3 kwa Serikali ikiwa ni shukrani kwa kuanza makubaliano mapya yenye tija.
Katibu Mkuu Bw. Doto James, alisema kuwa Serikali iliona vema fedha hizo zipelekwe kujenga hospitali ya Uhuru Mkoani Dodoma ambayo inatarajiwa kumalizika mwezi Oktoba mwaka huu.