Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imeshindwa kumteua Maalim Seif Sharif Hamad kugombea urais wa Zanzibar kupitia chama cha ACT-Wazalendo baada ya kuwekewa pingamizi.
Alhamisi tarehe 10 Septemba 2020, ZEC imewateua 16 kati ya 17 waliochukua fomu na kurudisha kugombea urais wa visiwa hivyo katika uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 27 na 28 Oktoba 2020.
Mkurugenzi wa Uchaguzi, Thabiti Faina, amesema, Maalim Seif ameshindwa kuteuliwa kutokana na vyama viwili vya DP na Demokrasia Makini kumwekea pingamizi.
Amesema, mapingamizi ya vyama hivyo yanafanana na yanahusu ujazwaji wa fomu za Maalim Seif kutokuwa sahihi.
Mkurugenzi huyo amesema, baada ya Maalim Seif kujibu mapingamizi hayo, tume hiyo itaamua kama ni kumteua au la.
Maalim Seif ndiye mgombea pekee anayewamia kugombea nafasi hiyo mara sita kati ya wote 17 waliojitosa kumrithi Rais Ali Mohamed Shein ambaye anamaliza muda wake kwa mujibu wa Katiba.