NEWS

10 Septemba 2020

Mwalimu Auawa kwa Kupigwa Risasi Nyumbani Kwake



Mwalimu wa Shule ya Sekondari Kihenya, wilayani Kasulu mkoani Kigoma, ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi akiwa nyumbani kwake.


Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, ACP James Manyama, alisema tukio hilo limetokea Septemba 6, majira ya saa tatu usiku, baada ya watu hao kuvamia nyumba ya mwalimu Fredrick Richard (30), aliyekuwa akiishi na mke na watoto wawili.


Alisema watu hao hawakuongea neno lolote baada ya kuingia ndani, walimpiga risasi mwalimu huyo na kuondoka bila kuchukua kitu chochote.


Jeshi hilo linamshikilia mtu mmoja akihusishwa na mauaji hayo baada ya polisi kuokota kofia katika eneo la tukio iliyosaidia kumpata mtuhumiwa huyo huku watuhumiwa wengine wakiendelea kutafutwa ili waunganishwe na mwenzao.


Kamanda alisema huenda tukio hilo ni la kulipa kisasi kwa kuwa wahalifu baada ya kutekeleza mauaji hawakuiba, hivyo kuwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi.