MENGI yamesemwa juu ya mahaba mapya na shatashata ya staa wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ na mkewe Amina Khaleef, yaliyoibuka wakiwa jijini Arusha, wikiendi iliyopita, ambapo sababu tatu za jamaa huyo kurejea kwa mkewe huyo, zikitajwa.
Kabla ya hapo, yalisemwa mengi ikiwemo ishu ya wawili hao kutengana, ambapo Amina alikuwa kwao jijini Mombasa, Kenya wakati Kiba akikatiza ‘aloni’ kwenye mitaa ya nyumbani kwake pale Tabata-Sanene jijini Dar.
Kuonekana kwa wawili hao wakiwa na furaha na mahaba kama yote, kumeibua shangwe kwa mashabiki wa mfalme huyo wa Bongo Fleva, ambapo wamemsifia kwa kitendo chake hicho cha kuamua kurejesha majeshi kwa mama wa mtoto wake, Keyaan Ali Kiba.
Kiba amekuwa staa wa kuweka siri mno juu ya maisha yake ya kifamilia, jambo ambalo liliwaaminisha wengi kwamba, hawako pamoja, lakini sasa wambeya limewashuka.
Tangu kuibuka kwa tetesi za Kiba kuachana na Amina, Februari, mwaka huu, jamaa huyo amekuwa akikanusha habari hizo bila mafanikio kwa sababu hakuwahi kuachia video wala picha za kimahaba na mwenzake huyo, lakini sasa watu wameelewa, kwani picha na video za kimahaba, zimejaa tele kwenye kurasa za habari za burudani mitandaoni.
Kwa mujibu wa mtu wa karibu wa familia ya Kiba na Amina, kuna sababu takriban tatu zilizomsukuma jamaa huyo kurejesha mahaba kwa mkewe kama zamani.
“Sababu ya kwanza kabisa ni mtoto. Unajua Kiba hataki mwanaye Keyaan alelewe na mzazi mmoja kama ilivyotokea kwa watoto wake wengine watatu aliozaa na wanawake tofauti.
“Kiukweli Kiba humuambii kitu kwa mwanaye Keyaan, maana hata kwenye ukurasa wake wa Instagram, ndiye mtu pekee ambaye amem-follow.
“Hakuwa tayari kuendelea kuwa mbali na mwanaye ambaye sasa ana umri wa zaidi ya miaka miwili. “Sababu ya pili ni kwamba, si rahisi kwa Kiba kumpata mwanamke mwenye sifa zake za uzuri kama Amina.
“Ukimtazama Amina hata kwenye picha zilizosambaa mitandaoni akiwa na Kiba, utagundua kuwa uzuri wake ni wa asili na siyo wa kutengeneza; yaani siyo feki kama walivyo wanawake wengi wa Kibongo.
Amina amebeba maana halisi ya uzuri wa mwanamke na tabia, hivyo kaka yetu (Kiba) hawezi kumwacha hivihivi, maana sidhani kama anaweza kupata mbadala wake.
“Sababu ya tatu, Amina siyo mtu wa kushinda na kukesha kwenye mitandao ya kijamii kama walivyo wanawake wengi ambao kazi yao huwa ni kufuatilia umbeya.
Tangu Amina aingie kwenye uhusiano na Kiba, ambapo kwa mrembo mwingine angefanya matangazo kwenye mitandao ya kijamii hadi dunia nzima ijue, lakini Amina yeye hakuwahi kufanya hivyo na ndivyo Kiba anavyotaka, kwani hapendi kuanika mambo yake ya chumbani hadharani,” kilisema chanzo chetu ambacho ni Team Kiba wa kutupwa.
Kuhusu kuachana na mkewe huyo, Kiba aliwahi kuliambia gazeti hili kuwa; “Sijaachana na mke wangu kama ambavyo watu wanadai, bali nilimruhusu aende kwao nchini Kenya kufanya kazi.
“Mimi na mke wangu hatujawahi kugombana wala kupishana kauli, siwezi kumuacha kwa kuwa ninampenda sana mke wangu.”
Kiba alifunga ndoa na Amina, asubuhi ile ya Aprili 19, 2018 mjini Mombasa, Kenya kisha kufuatiwa na bonge la sherehe pale Serena Hotel jijini Dar, ambayo ilimhusisha pia mdogo wake Kiba, Abdu Kiba ambaye naye alifunga ndoa, hivyo kuwa sherehe ya pamoja.
STORI SIFAEL PAUL, Risasi