NEWS

10 Septemba 2020

Takukuru Manyara yasaidiana na Wananchi Kurejesha Fedha zilizoporwa.

Na John Walter-Manyara
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, imekabidhi hundi  ya Shilingi Milioni 2,205,000 kwa Mkuu wa wilaya hiyo Mhandisi Zephania Chaula.

Hundi hiyo imekabidhiwa na  afisa wa TAKUKURU Wilaya ya Simanjiro Mhandisi Stephano Ghula mara baada ya kufanikiwa kuzirejesha fedha zilizokuwa zimefanyiwa ubadhirifu na aliyekuwa  Mtendaji wa Kijiji cha Lormorijoi,  Idd Mohammed Chiko.

Aidha Mkuu wa Wilaya alizikabidhi fedha hizo kwa  mtendaji wa kijiji cha Lormorijoi  Bi. Mary ambaye alipokea kwa niaba ya wanakijiji waliokuwa wamekusanyika ili kushuhudia jambo hilo lililofanikishwa na Takukuru.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Takukuru mkoa wa Manyara Holle Makungu imeeleza kuwa, awali kampuni ya Eshkesh Safari iliombwa  kutoa fedha hizo kwa ajili ya kuchangia shughuli za maendeleo kijijini hapo lakini hazikutumika kama ilivyokusudiwa.

Makungu amesema  walipokea  taarifa ya ubadhilifu wa fedha hizo kutoka kwa wananchi ambapo walifuatulia ambapo walimtaka  mtuhumiwa huyo  kuzirejesha na alifanya hivyo.

Takukuru mkoa wa Manyara inawapongeza wanakijiji wa Lormorijoi kwa kutokubali kufumbia macho kitendo hicho cha  ubadhirifu wa mali ya kijiji.

Holle Makungu ametoa rai kwa Wananchi katika vijiji vingine mkoani Manyara kuiga mfano huo kwa kutoa taarifa kwa ofisi ya TAKUKURU iliyo karibu au kwa namba ya dharura 113 ambayo mwananchi halipii gharama yoyote.