NEWS

10 Septemba 2020

Yafahamu Majimbo ambayo NEC imeyatolea maamuzi


Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imezipitia, kuzichambua na kuzifanyia maamuzi rufaa 34, ambazo kati ya hizo imekubali rufaa 13 na kuwarejesha wagombea wa majimbo 9 na imekataa rufaa 7 za wagombea ambao hawakuteuliwa, huku pia ikikataa rufaa 14 za kupinga walioteuliwa.

Taarifa hiyo imetolewa hii leo Septemba 9, 2020, na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Dkt Wilson Mahera, ambapo ameyataja majina ya majimbo ambayo rufaa 13 imezikubali ikiwemo Singida Magharibi, Madaba, Ilemela, Namtumbo,  Bagamoyo, Liwale, Tunduma, Bukene na Kigamboni.

Aidha mbali na kukubali rufaa hizo 13, pia imekataa rufaa 7 za wagombea ambao hawakuteuliwa, rufaa hizo ni kutoka kwenye Majimbo ya Singida Magharibi, Bahi, Handeni Vijijini, Madaba, Singida Mashariki, Ileje, Meatu na Bukene.

Mbali na hizo NEC pia imekataa rufaa 14, za kupinga walioteuliwa kutoka katika majimbo ya Igunga, Mwanga, Mafinga, Ilala, Manonga na Kisesa.

Idadi hiyo ya leo inafanya jumla ya rufaa za wagombea Ubunge zilizofanyiwa uamuzi na Tume kufikia 89, Tume itaendelea kutoa matokeo baada ya usajili na uchambuzi wa rufaa hizo kila siku na wahusika wa rufaa hizo watajulishwa