NEWS

28 Januari 2021

Rais Magufuli amsamehe Mkurugenzi Kahama


Rais John Magufuli amemsamehe Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kahama, Mkoani Shinyanga, Tanzania,  Anderson Msumba kwa kosa alilokuwa akichunguzwa la ununuzi wa gari la kifahari ikinyume na utaratibu, akisema amefanya kazi kubwa katika ambayo pia ameipandisha kuwa Manispaa ya Kahama.

Akizungumza leo Alhamaisi Januari 28, 2021, katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani humo, Rais Magufuli amesema amefurahishwa na miradi aliyoikagua inayotekelezwa kwa fedha za ndani za manispaa hiyo mpya.

“Nilianza kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi ya Halamshauri ya Wilaya utakaogharimu Sh1.8 bilioni. Nilipata bahati ya kupata maelezo ya wahandisi akina mama waliojenga. Kilichonifurahisha zaidi, ofisi ile inajengwa kutokana na mapato ya ndani ya Halmashauri,” amesema Rais Magufuli.

“Nikaambiwa jengo hilo limejengwa kwa mapato ya ndani aya halmashauri hii. Nikawa namwangalia mkurugenzi, alikuwa na ka- tuhuma kidogo ka - kujinunulia gari, nikasema kama fedha na kupitia madiwani wamejenga hili jengo la Sh1.8 bilioni, wanajenga jengo la hospitali kubwa tu la Sh3.2 bilioni, ngoja nione mpaka mwisho.

“Nikaenda kwenye kiwanda, nikaona ni maviwanda yale yale niliyoyaona Ulaya, nasema kwa dhati kwa sababu viwanda vinavyojengwa Ulaya ni hivyohivyo. Nilipopewa taarifa pale, nikaambiwa ardhi hii yote ilitolewa na halmashauri ni ekari 90 bure. Nikajiuliza sana. Nataka niwambie ndugu zangu kwamba huyu mkurugenzi na madiwani wana akili sana,” amesema Rais Magufuli.

Akaongeza kuwa kitendo cha kutoa eneo la uwekezaji bure na kutengeneza ajira zitakazoleta kodi ni cha akili kubwa.

“Ukishatoa ajira na kukusanya kodi ukaongeza mzunguko wa fedha katika eneo moja, ile ni busara kubwa sana, kwa hiyo nimeamua kumshamehe mkurugenzi huyu na hili gari namrudishia aendelee kuliendesha, lakini asirudie tena kununua magari nje ya utaratibu wa sheria.

“Nasema kwa dhati sitaki kuwa mnafiki. amefanya makubwa. Mkurugenzi hongera sana. Najua unapigwa vita wanaokupiga vita sasa wakuogope kwamba unafanya kazi nzuri. Ninahitaji watu wa aina hii, kakosa kale kadogo  kamefuta dhambi zake,” amesema Rais Magufuli.