NEWS

29 Januari 2021

Rais Magufuli Apongeza Wizara Ya Kilimo Kwa Mkakati Wa Uzalishaji Ngano


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameipongeza Wizara ya Kilimo kwa kuweka mkakati wa kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa ngano huku akiagiza mashamba yote yaliyokuwa ya serikali na sasa hayatumiki kuzalisha ngano yawekewe utaratibu wa kugawiwa kwa wakulima.


Rais Magufuli ametoa maagizo hayo jana (28.01.2021) Chapulwa mjini Kahama wakati alipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda cha vinywaji baridi na vifungashio vinavyomilikiwa na kampuni ya KOM Group ya wazawa chini ya Mtanzania Mhoja Nkwabi.


” Nimefurahi kuona Wizara ya Kilimo imeanza kuweka mkazo kwenye uzalishaji wa ngano ili suala la kuagiza zaidi ya tani milioni moja nje ya nchi na kufanya nchi itumie fedha nyingi za kigeni liishe” alisema Rais Dkt. Magufuli.


Aidha ,Rais Dkt. Magufuli ameagiza mashamba yote yaliyokuwa ya serikali yaliyokusudiwa kwa kuzalisha ngano na sasa hayalimwi, wizara ya kilimo ihakikishe wamiliki wake wanayalima vinginevyo  yagawiwe kwa wawekezaji wenye uwezo na wakulima wadogo.


“Yale mashamba yasiyotumika kuzalisha ngano na ni ya serikali tuyalime yote, wawekezaji wapewe kulima ngano hata ikibidi tuyatoe bure” aliagiza Rais Dkt. Magufuli.


Awali akizungumza kwenye halfa hiyo Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda alimpongeza Rais  Magufuli kwa uthubutu wake na maelekezo yake kuhusu nchi kujitosheleza kwa zao la ngano na kuahidi wizara itaendelea kutekeleza maagizo ya Rais.


Prof Mkenda alieleza kuwa kwa sasa nchi inazalisha wastani wa tani 60,000 za ngano huku ikiingiza toka nje tani takribani milioni moja kwa mwaka  wakati Tanzania ina ardhi nzuri inayofaa kwa uzalishaji zao hilo ndio maana Wizara yake imeweka mkakati maalum wa kuhakikisha baada ya miaka miwili nchi inajitosheleza kwa ngano hapa .


“Tumekubaliana na wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa wa ngano kwa hiari kuwa kuanzia mwaka huu wataanza kununua ngano ya wakulima wa ndani kwa bei ya Shilingi 800 kwa kilo na kama wataagiza nje kiwango cha asilimia 60 basi watapaswa kununua kiwango kama hicho hapa nchini ili kutoa fursa kwa wakulima kupata soko “ alisisitiza Prof. Mkenda.


Katika hatua nyingine Prof. Mkenda amemweleza Rais Magufuli kuwa Wizara ya Kilimo itashirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara kutafuta soko la uhakika la mchele wa wakulima wa Kahama ambao ni wazalishaji wakubwa .


Prof. Mkenda aliongeza kusema Wizara ya Kilimo inauona mji wa Kahama kuwa ni kituo maalum cha kiuchumi kwa kuwa ipo karibu na mipaka ambayo ikitumika vizuri itasaidia kutoa fursa ya masoko ya mazao ya kilimo .


Waziri huyo wa Kilimo amewapongeza kampuni ya KOM Group kwa uwekezaji utakaotoa fursa ya mazao ya kilimo ikiwemo maembe, machungwa, mapera  na mazao ya mpunga na mahindi kuongezwa thamani pia ajira zaidi ya 400 za kudumu na 1000 za muda.


“Baadhi ya mpunga wetu unavuka mipaka na kwenda kuchakatwa huko badala ya hapa Kahama, hivyo tunahitaji kuona wawekezaji wengi kama KOM Group wakianzisha viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo na kuyasindika hapa nchini ili wakulima wanufaike na kuwa uhakika wa kipato” alisema Prof. Mkenda.


Naye Waziri wa Viwanda na Biashara Cecil Mwambe amekishauri kiwanda cha KOM Group cha Kahama kutumia fursa ya uwepo wa korosho ghafi nyingi nchini kuanza kuchakata bidhaa zitokanazo na korosho kwani zina soko kubwa ndani na nje.


“Wananchi wa Kahama  tumieni fursa ya kiwanda hiki cha KOM Group kuuza malighafi ili kuongeza kipato na uwezo wa kiwanda kuzalisha bidhaa hali itakayokuza uchumi wa nchi “ alisema Mwambe


Rais Dkt. John Pombe Magufuli yuko ziarani Mkoa wa Shinyanga kukagua shughuli za maendeleo pamoja na kuongea na wananchi.


Mwisho.
Imeandaliwa na ;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo
KAHAMA
28.01.2021